Vwawa FM Radio
Vwawa FM Radio
May 27, 2025, 9:52 am

Ukosefu wa vyoo katika vituo vya bodaboda wazua hofu ya uchafuzi wa mazingira katika mkoa wa Songwe
Na Mkaisa Mrisho
Waendesha pikipiki (bodaboda) katika maeneo mbalimbali ya Vwawa, mkoani Songwe, wamelalamikia ukosefu wa vyoo katika vituo vyao vya kazi, wakisema hali hiyo inaweza kuchangia uchafuzi wa mazingira. Kwa kiasi kikubwa, wanategemea vyoo vya majirani au kutumia maeneo ya wazi kupata huduma hiyo muhimu.
Wakizungumza Mei 19, 2025, baadhi ya waendeshaji kutoka vituo vya Kwa Chaula na Kona ya Mkoa wamesema kuwa changamoto hiyo inawalazimu kutafuta huduma ya choo katika nyumba za jirani, kwenye choo cha kulipia (chocho), au hata maeneo yasiyo rasmi.
Sambamba na malalamiko hayo, wametoa wito kwa wadau wa sekta ya afya kujitokeza na kusaidia kutatua changamoto hiyo, wakisisitiza kuwa upatikanaji wa vyoo katika vituo hivyo ni hatua muhimu ya kuboresha usafi wa mazingira na afya kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Pikipiki Mkoa wa Songwe, Omari Mbuba, ametoa wito kwa mamlaka husika kuweka mpango maalum wa kuhakikisha kila kituo kinakuwa na choo maalumu huku akisisitiza umuhimu wa kudumisha usafi katika maeneo ya kazi ya waendeshaji hao.