Savvy FM

Wananchi 1,200 Arusha wanufaika na matibabu ya moyo bure

January 6, 2026, 5:10 pm

Mkuu wa Mkoa wa Arusha CPA Amos Makala akizindua programu ya matibabu.Picha na Mariam Mallya

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, amekagua na kuzindua kitengo cha programu ya vipimo na matibabu bure kwa magonjwa ya moyo inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Arusha Lutheran Centre (Seliani), mkoani Arusha.

Na Mariam Mallya

Akizungumza na wananchi pamoja na watoa huduma za afya, Makalla amesema jumla ya wananchi 1,200 wamenufaika na huduma hiyo ya vipimo na matibabu bure. Ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuwawezesha wananchi wasiokuwa na uwezo, hususan wale watakaopatiwa rufaa ya kwenda kupata matibabu zaidi katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) mkoani Dar es Salaam. Aidha, amewahamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya kwa wote ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa urahisi na kwa wakati.

Sauti ya CPA Amos Makalla,Mkuu wa Mkoa wa Arusha

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Peter Kisenge, amesema kwa sasa kuna takribani vituo sita nchini vinavyotoa huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo, hali inayochangia kusogeza huduma hizo karibu zaidi na wananchi.

Sauti ya Peter Kisenge,Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete

Sambamba na hayo, wananchi wa Mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani waliopatiwa huduma za vipimo na matibabu wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwezeshaji wake wa programu ya vipimo na matibabu bure kwa magonjwa ya moyo inayofanyika kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Arusha Lutheran Centre (Seliani).

Sauti za Wananchi waliopatiwa matibabu