Savvy FM
Savvy FM
September 29, 2025, 5:40 pm

Wananchi wa Mitaa miwili ya Roman Katoliki (RC) na Mbeshere pamoja na viongozi wa Kata ya Oloirieni jijini Arusha, wamefanya kikao cha dharura kujadili tukio la hivi karibuni la maandamano yaliyofanywa na wananchi kuhusu tuhuma mbalimbali dhidi ya mwanamke mmoja anayefahamika kwa jina Nice Misheri maarufu kama Chinaa.
Na Jenipha Lazaro
Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na viongozi wa serikali ya mtaa, viongozi wa dini, pamoja na wananchi wenyewe, malalamiko mbalimbali yaliibuliwa, ikiwemo madai ya unyanyasaji, uporaji wa fedha, na kubambikiziwa bili kubwa zisizoeleweka kwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo.
Kwa upande wake, Nice Misheri maarufu kama Chinaa, amekanusha tuhuma hizo na kusema kuwa yeyote mwenye ushahidi wa tuhuma hizo pamoja na ripoti ya polisi (RB), ajitokeze hadharani.
Viongozi wa mitaa hiyo kwa kushirikiana na mtendaji wa Kata ya Oloirieni, wamewataka wananchi kuwa na subira na kutoa ushirikiano wakati huu ambapo wanajiandaa kukaa kwenye kikao maalum cha ulinzi na usalama wa Kata, ili kujadili kwa kina sakata hilo na kutoka na maamuzi yenye maslahi ya pande zote.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi kupitia Inspekta Nyamweru Andrea Kasato, amewatahadharisha wananchi dhidi ya kujichukulia sheria mkononi, na kusisitiza kuwa mamlaka za usalama zinaendelea kulifanyia kazi suala hilo kwa mujibu wa sheria na taratibu.