Savvy FM

Zoezi maalum la kuvalisha tembo mikanda ya GPS laanza Mkomazi

September 23, 2025, 7:03 pm

Picha ya tembo akiwekewa GPS.Picha na Jenipha Lazaro

Taasisi ya utafiti wa wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kwa kushirikiana na Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania (TAWA) na Mamlaka ya hifadhi za Taifa (TANAPA), imeanza zoezi maalum la kuvalisha tembo mikanda ya mawasiliano katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, mkoani Tanga. Lengo kuu la zoezi hilo ni kudhibiti mienendo ya tembo ili wasivamie makazi ya watu na kusababisha madhara kwa binadamu na mali zao.

Na Jenipha Lazaro

Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Mkurugenzi wa Wanyama Pori nchini, Alex Lobora, amesema teknolojia hiyo inalenga kupunguza migongano baina ya binadamu na tembo, ambayo imekuwa ikisababisha uharibifu mkubwa wa mazao na wakati mwingine kuhatarisha maisha ya watu.

Sauti ya Alex Lobora,Mkurugenzi wa Wanyama Pori nchini

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Dkt. Eblate Mjingo, amesema kuwa mbali na kutumia teknolojia ya GPS, jamii zinazoishi jirani na hifadhi pia zinafundishwa mbinu bora za kufukuza tembo kwa njia salama na zisizohatarisha maisha yao.

Mafunzo hayo yanahusisha matumizi ya mbinu rafiki kwa mazingira kama vile mizinga ya nyuki, pilipili, na fataki.

Sauti ya Dkt. Eblate Mjingo,Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI

Hata hivyo, wakazi wa maeneo hayo, hususani wilayani Korogwe, wamesema kuwa tatizo la tembo limekuwa changamoto kubwa katika maisha yao ya kila siku.

Wengi wameshindwa kufanya kazi za kilimo kwa amani kutokana na hofu ya kuvamiwa na tembo. Wameeleza kuwa ujio wa mradi huu umewapa matumaini mapya ya kurejea kwenye shughuli zao za kiuchumi bila hofu.

Sauti ya mwananchi wa Korogwe