Savvy FM
Savvy FM
September 18, 2025, 10:26 pm

Baada ya changamoto ya muda mrefu ya kutokuwepo kwa huduma ya upasuaji kwa wajawazito, Kituo cha Afya cha Ngarenaro mkoani Arusha kimezindua rasmi huduma hiyo muhimu, hatua inayolenga kuokoa maisha ya mama na mtoto wakati wa kujifungua.
Na Jenipha Lazaro
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dkt. Antony Mao, amesema kuwa kabla ya maboresho hayo, wanawake waliokuwa wanahitaji upasuaji walikuwa wakipelekwa kwenye vituo vya jirani, hali ambayo ilihatarisha maisha yao kutokana na ucheleweshaji wa huduma.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Jiji la Arusha, Dkt. Maduhu Dindwa, amesema zaidi ya shilingi milioni 300 zimetumika katika kuboresha kituo hicho, ikiwemo ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa.
Nao baadhi ya wakina mama waliopatiwa huduma katika vyumba hivyo wameishukuru serikali kwa jitihada zake katika kuboresha huduma za afya, nakusema hatua hiyo ni ya kupongezwa kwani itapunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya mama na mtoto vinavyotokana na matatizo ya uzazi.
Kituo cha Afya Ngarenaro sasa kinakuwa kituo cha kumi (10) katika Jiji la Arusha kutoa huduma za upasuaji, huku serikali ikipanga kuongeza idadi ya vituo vinavyotoa huduma hiyo ili kufanikisha lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.