Savvy FM
Savvy FM
August 21, 2025, 11:15 pm

Zaidi ya madawati 90 yamekabidhiwa katika shule ya sekondari ya Embris, iliyopo Kijiji cha Landanai, Kata ya Naberera, Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara.
Madawati hayo yametolewa na shirika lisilo la kiserikali la World Vision kwa lengo la kuiunga mkono serikali ya awamu ya sita katika jitihada zake za kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Na Jenipha Lazaro
Meneja wa mradi kutoka World Vision Wilaya ya Simanjiro, Samuel Charles, amesema kuwa shirika hilo linaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya hiyo, ikiwemo miradi miwili ya muda mfupi inayolenga kutunza mazingira na kuhimiza ujumuishaji wa watu wenye ulemavu katika jamii.
Kwa upande wake, kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Mwalimu Marco Masala, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, amewashukuru World Vision kwa msaada huo na kusisitiza kuwa halmashauri itaendelea kushirikiana na wadau wote wa maendeleo katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu.
Naye, Matayo Milya, akizungumza kwa niaba ya wazazi, aliipongeza World Vision na kutoa wito kwa wadau wengine kuendelea kusaidia shule hiyo ili kufanikisha azma ya kuinua elimu kwa watoto wa eneo hilo.
Wanafunzi wa shule hiyo pia walieleza baadhi ya changamoto wanazokumbana nazo, zikiwemo ukosefu wa mabweni na nishati ya umeme, hali inayovuruga mazingira ya kujisomea hasa nyakati za usiku.