Vwawa FM Radio
Vwawa FM Radio
June 9, 2025, 1:39 pm

Mitazamo hiyo ni ya kutowathamini kwa maumbile yao
Na Stephano Simbeye
Mitazamo hasi dhidi ya watu wenye ulemavu imeendelea kuwa mojawapo ya sababu zinazochangia kutowajumuisha ipasavyo katika shughuli za maendeleo ya jamii, hali inayosababisha vipaji vyao walivyopewa na Mungu kubaki bila kuendelezwa.
Kauli hiyo imetolewa Juni 6 mwaka huu na mwalimu wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu kutoka Shule ya Msingi Mwenge, Magreth Ndunduru, wakati wa mafunzo ya lugha ya alama yaliyotolewa kwa watoa huduma za afya.
Mafunzo hayo ya siku mbili yameandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la ADP Mbozi kwa kushirikiana na shirika la DSW chini ya mradi wa SAfA, na kufanyika katika ukumbi wa Simple Palace, uliopo mjini Vwawa, wilayani Mbozi, mkoani Songwe.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Mkoa wa Songwe, Abel Mwakajila, amesema bado zipo changamoto nyingi zinazowakabili watu wenye ulemavu wanapotafuta huduma za kijamii, ikiwemo ukosefu wa miundombinu rafiki na ugumu wa kufikika kwa maeneo muhimu.
Mwakajila pia ametoa wito kwa taasisi zote za umma na binafsi kuhakikisha zinarekebisha au kujenga miundombinu rafiki kwa wenye ulemavu, ili waweze kupata huduma kwa usawa.