Uyui FM
Uyui FM
12 February 2026, 11:04 pm
Na Zaituni Juma

Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wilaya wa Tabora, leo Februari 12, 2026 imetembelea Kituo cha Afya Mailitano kata ya Ipuli, katika wodi ya mama na mtoto na kutoa misaada mbalimbali kwa akina mama wanaopatiwa huduma kituoni hapo.
Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Tabora, Mwl. Kulwa Kavula, akiongozana na viongozi na wanachama wa CCM wilaya ya Tabora, ameeleza wamefika kituoni hapo kwa lengo la kuwajulia hali wazazi waliojifungua na kuwapatia mahitaji muhimu kwa ajili ya uangalizi wa watoto wao ambapo sambamba na mambo hayo wamepanda miti ya matunda ili kutunza mazingira ya kituo hicho.

Mgeni rasmi ambaye ni Afisa Maendeleo wilaya ya Tabora, Tumaini Mgaya amepongeza jitihada za UWT kwa kutembelea kituo hicho na kupanda miti ambayo itakuwa na faida kwa watumiaji wa huduma za afya kituoni hapo huku akiahidi kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora inaongeza juhudi kuhakikisha ujenzi wa majengo mapya unaoendelea, unamalizika kwa wakati.


Wakizungumza na UFR, akina mama waliopokea misaada kutoka UWT wameshukuru na kupongeza uwepo wa kituo hicho cha afya umewasaidia wananchi wa Tabora kwani huduma zinazotolewa ni nzuri.
