Uyui FM

Barabara Usoke hadi Tutuo wilayani Urambo kujengwa kiwango cha lami

11 June 2025, 6:22 pm

Baadhi ya wananchi walioshiriki kwenye mkutano ofisi ya Tarafa Usoke.Picha na Agustino Florian

”Ni muda mrefu nimekuwa nikiisemea barabara hii Bungeni na kukamilika kwake kutaleta manufaa makubwa kwa wananchi”Mbunge Margaret

Na Mwandishi wetu Agustino Florian

Serikali kupitia wakala ya barabara Tanzania- TANROADS imeanza utekelezaji wa mradi wa barabara yenye urefu wa kilomita 69 kutoka kata ya Usoke wilayani Urambo hadi Tutuo wilayani Sikonge kwa kiwango cha lami.

Mbunge wa jimbo la Urambo Margaret Sitta akiambatana na timu ya wataalamu wa halmashauri ya wilaya ya Urambo ikiongozwa na mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri Grace Quintine wameshiriki mkutano wa hadhara uliofanyika katika ofisi za Tarafa ya Usoke kwa lengo la kumtambulisha Mhandisi wa barabara hiyo.

Wakati wa kumtambulisha, mhandisi wa mradi huo Mbunge Margaret amesema kwamba kukamilika kwa barabara hiyo kutaleta manufaa makubwa kwa wananchi.

Mbunge wa jimbo la Urambo akizungumza na wananchi.Picha na Agustino Florian

Meneja wa wakala ya barabara Tanzania- TANROADS Mkoa wa Tabora Mhandisi Rafael Mlimaji amesema wameanza hatua za awali za utekelezaji wa mradi huo, inayogharimu zaidi ya shilingi milioni 605.

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Urambo Grace Quintine amewataka Wananchi kutoa ushirikiano wakati wa utekelezwaji wa mradi huo na kuongeza kuwa wilaya ya Urambo imepokea zaidi ya shilingi bilioni 40 kwaajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. 

Mkurenzi mtendaji halmashauri ya wilaya ya Urambo akieleza utekelezaji wa mradi.Picha na Agustino

Nao wananchi wa kata za Usoke Shabani Rashidi na Saidi Mahenga wamesema wameupokea mradi huo kwa mikono miwili, utakaoenda kutatua changamoto ya usafirishaji wa bidhaa na kuomba kuwekewa taa za barabarani.