Savvy FM
Savvy FM
27/02/2026, 15:51

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha (DC ),Bwn Sulemani Msumi, amesema halmashauri inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa watumishi wake, ikiwemo walimu, hususan katika kata za pembezoni kwa kuwajengea nyumba za kuishi.
Na Mariam Mallya
Amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Arusha DC imefanikiwa kujenga nyumba za walimu katika shule nne zilizopo katika kata tofauti, hatua inayolenga kupunguza kero ya walimu kutembea umbali mrefu kwenda kutoa huduma kwa wanafunzi.
Aidha, amesema katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu, halmashauri imetenga shilingi milioni 40 kwa ajili ya Shule ya Sekondari Likamba, kwa ukamilishaji wa nyumba tatu za walimu. Ameeleza kuwa zoezi hilo ni endelevu na litanufaisha si walimu pekee bali pia watumishi wengine wa halmashauri hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha Dc, Baraka Mesiaki, amesema katika kikao hicho cha baraza la kawaida (Full Council), madiwani walijadili mada mbalimbali zinazogusa maendeleo ya wananchi katika kata zote 27 za halmashauri hiyo.
Amesema miongoni mwa ajenda zilizopewa kipaumbele ni maboresho ya utoaji wa mikopo kwa wanawake, vijana na makundi maalum, ikiwemo namna ya kurejesha mikopo iliyochukuliwa na vikundi ambavyo baadhi ya wanachama wake walishindwa kurejesha kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo vifo vya baadhi ya wanavikundi.
Madiwani hao wamekubaliana kuunda kamati rasmi itakayowahusisha pia mabalozi wa mitaa, ili kuhakikisha vikundi vinavyokopa vinakuwa na taarifa sahihi na kumbukumbu kamili kupitia kwa balozi husika, kwa kuwa ni viongozi wanaowafahamu wananchi wao na wanaweza kurahisisha ufuatiliaji wa marejesho ya mikopo.
Katika hatua nyingine, halmashauri hiyo imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 600 katika kipindi cha nusu mwaka kuanzia Oktoba hadi Desemba 2025.