Savvy FM
Savvy FM
February 17, 2026, 2:44 pm

Punda nchini Tanzania wanakabiliwa na changamoto kubwa za ustawi, ikiwemo ukosefu wa lishe bora, huduma za afya pamoja na ulinzi dhidi ya vitendo vya utoroshaji na biashara haramu.
Na Mariam Mallya
Wataalamu wa mifugo na wadau wa ustawi wa wanyama wanasema hali hiyo inaathiri moja kwa moja shughuli za kiuchumi za kaya nyingi, hususan maeneo ya vijijini ambako punda hutumika kama nguvu kazi muhimu.
Akizungumza katika warsha iliyowakutanisha baadhi ya waandishi wa habari iliyoandaliwa na mashirika yasiyo ya kiserikali ya ASPA na Brooke East Africa mkoani Arusha, Mkurugenzi wa ASPA, Livingston Masija, amesema kuwa ili kuhakikisha uzalishaji na ustawi wa punda unaimarika, ni lazima wanyama hao wapatiwe chakula cha kutosha, chanjo pamoja na maeneo salama ya kulala.
Kwa upande wake, daktari wa wanyama kutoka shirika hilo, Dkt. Lazaro Mirama, amesema kuna umuhimu kwa serikali kuimarisha udhibiti wa mianya inayochochea utoroshwaji wa punda kwenda nje ya nchi, kwani vitendo hivyo vinapunguza idadi ya wanyama hao na kuathiri upatikanaji wake kwa wafugaji na watumiaji.
Naye Jastini Kimanga, daktari wa mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kituo cha uchunguzi kanda ya kaskazini, amesema serikali tayari ilishatoa tamko la kuzuia biashara, uchinjaji na utoroshwaji wa punda, hususan katika maeneo ya mipakani.
Ameongeza kuwa wataalamu wa mifugo wapo kazini kuhakikisha hakuna vibali vya kusafirisha punda.