Savvy FM
Savvy FM
January 4, 2026, 6:06 pm

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mheshimiwa Joseph Modest Mkude, ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha na maeneo jirani kuzingatia afya zao kwa kufanya uchunguzi wa mara kwa mara ili kuepukana na magonjwa yasiyo ya lazima, hususan magonjwa yasiyoambukiza.
Na Mariam Mallya
Mheshimiwa Mkude ameyasema hayo wakati alipotembelea kambi maalum ya matibabu jijini Arusha, iliyoanza tarehe 29 Desemba 2024, ambapo alieleza kuwa magonjwa ya moyo ni miongoni mwa changamoto kubwa za kiafya zinazowakumba wananchi wa mkoa huo.
Alieleza kuwa hadi kufikia tarehe 4 Januari 2025, wananchi takribani 800 wamepatiwa huduma za afya katika kambi hiyo, wakiwemo watu wazima 700 na watoto 100. Huduma zilizotolewa ni pamoja na vipimo maalum vya moyo kama ECHO na ECG.
Aidha, wagonjwa 53 waliokuwa na uhitaji wa upasuaji walifanyiwa uchunguzi na tathmini, ambapo upasuaji tano (5) umefanikiwa kufanyika kwa ushirikiano wa madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Dkt. Peter Kisenge, amesema kuwa hadi sasa taasisi hiyo imeendesha kambi sita za matibabu ya moyo katika maeneo mbalimbali nchini, huku akieleza kuwa kwa Jiji la Arusha wanaendelea kupanga mikakati ya kuboresha na kupanua huduma hizo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.