Savvy FM
Savvy FM
December 16, 2025, 4:07 pm

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, amewataka madiwani wa Jiji la Arusha kuhakikisha wanakusanya mapato na kusimamia kikamilifu miradi inayotekelezwa ndani ya Jiji ili iweze kukamilika kwa wakati. Akizungumza leo katika mkutano na Baraza la Madiwani na Menejimenti ya Jiji la Arusha, Makalla alisisitiza umuhimu wa usimamizi wa miradi mikubwa kama vile uwanja wa mpira, stendi kubwa ya mabasi, na soko la Kilombero ili kumaliza kwa wakati na kuleta manufaa kwa jamii.
Na Mariam Malya
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alitahadharisha kuwa madiwani wanapaswa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa mkaguzi na kufanya kazi kwa pamoja na kuchukua hatua juu ya taarifa watakazopewa na mkaguzi.
Katika upande mwingine, Makalla aliwataka madiwani kuwashukuru wananchi kwa kuwapigia kura na kwa imani waliyoionesha kwao, akisisitiza kuwa ni muhimu kwa madiwani kutekeleza ahadi walizozitoa kwa wananchi wakati wa kampeni. Aliongeza kuwa madiwani wanapaswa kwenda kwa wananchi ili kuwashirikisha na kusikiliza changamoto zao, kwani wananchi wanapenda kuelezwa na kuhusishwa katika maendeleo ya Jiji lao.