Savvy FM
Savvy FM
July 23, 2025, 11:46 pm

Watendaji wa uchaguzi katika mikoa ya Arusha na Manyara wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria walizofundishwa, kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Na Jenipha Lazaro
Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo ya wasimamizi wa uchaguzi kwa mikoa ya Arusha na Manyara, Mwenyekiti wa mafunzo hayo, Bw. Shabani Fernandi, amewataka watendaji wa uchaguzi kuhakikisha kuwa wanafuata kwa umakini maelekezo waliyopewa kuhusu usimamizi wa uchaguzi.Bw. Fernandi amesema kuwa matumizi sahihi ya fedha za uchaguzi na usimamizi wa vifaa ni jukumu la kisheria kwa wasimamizi hao, na hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na weledi wa hali ya juu.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bi. Zakia Abubakari, amewakumbusha wasimamizi hao kuwa wamekula viapo vya kutunza siri za uchaguzi, na hivyo hawapaswi kutoa taarifa yoyote isiyoidhinishwa na Tume.
Mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wa mwaka huu, ambapo Tume ya Uchaguzi inalenga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki, amani na kwa kuzingatia sheria za nchi.