Tanzania yapokea wakimbizi 11,049 toka DRC ndani ya miezi mitano
July 3, 2023, 12:43 pm
Mkurugenzi idara ya huduma kwa wakimbizi nchini Tanzania Bw. Suddy Mwakibisa amesema serikali ya Tanzania imepokea waomba hifadhi 11,049 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Mei 30 2023.
Na; Amina Semagogwa
Serikali ya Tanzania kupitia kambi ya wakimbizi Nyarugusu imepokea jumla ya waomba hifadhi 11,049 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Mei 30, 2023.
Mkurugenzi idara ya huduma kwa wakimbizi nchini Tanzania Bw. Suddy Mwakibisa amesema idadi hiyo ya wakimbizi kutoka DRC kuingia nchini Tanzania inatokana na machafuko yanayoendelea nchini kwao.
Amesema hayo wakati akihutubia umati wa wakimbizi kwenye maadhimisho ya siku ya Mkimbizi Duniani hivi karibuni ambayo kitaifa yamefanyika katika kambi wakimbizi Nyarugusu wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Bw. Mwakibisa amesema kuanzia mwezi January hadi Mei ,2023 jumla ya wakimbizi 1,343 kutoka familia 527 wamerudi nchini Burundi kwa hiari.
Bw. Mwakibisa amesema Tanzania imekuwa ikipokea wakimbizi kwa miaka mingi na kwamba hadi kufikia sasa kambi za wakimbizi Nduta na Nyarugusu zina zaidi ya wakimbizi 260,000.
Ikumbukwe kuwa Juni 20 mwaka huu ilikuwa na siku ya Mkimbizi Duniani ambayo kitaifa imeadhimishwa katika kambi ya wakimbizi Nyarugusu wilayani Kasulu mkoani Kigoma ikiwa na Kauli mbiu ya ‘’ Matumaini mbali na nyumbani, ulimwengu unaojumuisha wakimbizi kila wakati’’.