Mtegani FM
Mtegani FM
19 September 2025, 1:16 pm

Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar (BPRA) umeeleza kuwa moja ya malengo yake makubwa ni kujitambulisha kwa wananchi na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kusajili biashara na mali rasmi visiwani.
Na Miraji Manzi Kae
Akizungumza na Kituo cha redio Mtegani Fm, Hamis Haji Bakari, Msaidizi Mrajis Nyaraka wa BPRA, amesema taasisi hiyo imekuwa ikihimiza wananchi kuona umuhimu wa kufanya usajili kwa sababu ni hatua ya kisheria na kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi.Amefafanua kuwa kusajili biashara na mali kunamwezesha mmiliki kupata uhalali wa kisheria, urahisi wa kufikia huduma za kifedha ikiwemo mikopo, na pia huongeza uaminifu kwa washirika wa kibiashara pamoja na wateja.
Aidha, Hamis Haji Bakari amesema BPRA inalenga kuondoa dhana kwamba usajili ni kwa ajili ya wafanyabiashara wakubwa pekee, akisisitiza kuwa hata wajasiriamali wadogo wadogo wanapaswa kusajili biashara zao ili kujihakikishia ulinzi na haki zao.BPRA imesema itaendelea kusogeza karibu huduma zake kupitia njia za kidigitali na kushirikiana na vyombo vya habari ili kuhakikisha elimu inawafikia wananchi wa mijini na vijijini kwa usawa.Hata hivyo, taasisi hiyo imetoa wito kwa wananchi wote, hususan vijana wenye ndoto za kijasiriamali, kuhakikisha wanajisajili ili kuchangia ustawi wa uchumi wa Zanzibar na kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na kutokuwa na usajili rasmi.