Mtegani FM

Vikundi vya wenye ulemavu na mafunzo ya biashara Kusini Unguja

11 September 2025, 4:34 pm

Picha ikionesha viongozi kutoka tamwa znz pamoja na shijuwaza na washiriki mbali mbali katika mafunzo ya siku 2 , Picha na Miraji Manzi Kae

Wanachama 25 kutoka vikundi 16 vya kuweka na kukopa katika Wilaya ya Kusini Unguja wamepatiwa mafunzo ya siku mbili ya kuchagua, kupanga na kusimamia biashara, chini ya Programu ya Mashirikiano ya Pamoja kwa ajili ya Haki za Watu wenye Ulemavu (CADiR).

Na Miraji Manzi Kae

Mafunzo hayo yametekelezwa na (TAMWA ZNZ), (SHIJUWAZA) na (ZANAB) kwa ushirikiano na Shirika la Watu Wenye Ulemavu la Norway (NAD). Kati ya washiriki hao, 16 ni watu wenye ulemavu na 9 ni walezi na wasimamizi wa watoto wenye ulemavu.Akifungua mafunzo hayo, Mratibu wa (CADiR) kutoka (NAD), Bi. Aziza Ismail, alisema lengo kuu ni kuwawezesha watu wenye ulemavu kuinuka kiuchumi kupitia biashara zenye tija. Naye mkufunzi Muhidini Ramadhan wa TAMWA ZNZ alisisitiza kuwa elimu ya ujasiriamali inaweza kupunguza umasikini kwa watu wenye ulemavu.

Meneja wa Programu (TAMWA ZNZ), Bi. Nairat Ali, alisema mafunzo hayo yatawasaidia wanachama kupanga na kuchagua biashara endelevu, huku Afisa Programu wa (ZANAB), Bw. Khamis Ali, akiwataka washiriki kutumia vyema fursa ya kupata mikopo.Washiriki walijifunza kuandaa mipango ya biashara ikiwemo kilimo, ufugaji, ushonaji na uendeshaji maduka. Kwa niaba ya wenzake, Yusra Ali Hassan wa kikundi cha Mtu ni Utu alishukuru waandaaji na kueleza kuwa wamepata mwongozo mzuri wa kusimamia fedha na kukuza biashara.Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa programu ya (CADiR) inayolenga kuimarisha vikundi vya kuweka na kukopa vya watu wenye ulemavu katika wilaya 11 za Unguja na Pemba.

Sauti Ya Mshiriki wa Mafunzo