Kagera Community Radio
Kagera Community Radio
June 21, 2025, 2:34 pm

Viongozi mbalimbali wilayani Muleba mkoani Kagera wametakiwa kushirikiana ili kudhibti vitendo vya kikatili kwa watoto ambavyo vimekuwa vikipelekea baadhi yao kushindwa kufikia ndoto zao.
Na. Anold Deogratias
Mkuu wa Wilaya ya Muleba mkoani Kagera Dkt. Abel Nyamahanga amewataka wadau wa maendeleo pamoja na viongozi mbalimbali kushirikiana kudhibiti vitendo vya kikatili kwa watoto ambavyo vimekuwa vikipelekea baadhi yao kushindwa kufikia ndoto zao.
Dkt. Nyamahanga amesema hayo kwenye maadhimisho ya Siku ya Mtoto Afrika ambayo kwa Wilaya ya Muleba yamefanyika Juni 16, 2025 katika kijiji cha Runazi kata ya Kasharunga.

Amesema kuwa katika wilaya ya Muleba imebainika kuwa jumla ya watoto 154 wamefanyiwa vitendo vya kikatili kwa kipindi cha mwezi Julai mwaka 2024 hadi Mei 2025 ambapo kati ya watoto hao 38 wamefanyiwa ukatili wa kingono, 17 ukatili wa kihisia, ukatili wa kimwili 91, na watoto 9 wametelekezwa na wazazi wao.
Awali akisoma Risala mmoja wa Watoto Kerine Senfolian ameomba Serikali ihakikishe sheria yakumlinda mtoto inatekelezwa na hatua kali za kisheria zinachukuliwa kwa wale watakaobainika kufanya vitendo vya kikatili pamoja na kuwaomba wazazi kuzingatia maadili ya kitanzania wakati wa malezi.
Kwa uapande wake mmoja wa wadau wa makuzi, malezi na maendeleo ya awali ya mtoto Bw.Abimeleck Richard amesema kuwa kuna vyanzo vingi vinavyosababisha ukatili kwa watoto ikiwemo imani potofu, umaskini na ukosefu wa uelewa juu ya haki za mtoto.
Nao baadhi ya wazazi na walezi walioshiriki hafla hiyo wamesema kuwa wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata shule imekuwa moja ya sababu ya ukatili kwa watoto kwani wanakutana na vishawishi vingi njiani.
Siku ya mtoto wa Afrika uhazimishwa kila ifikapo juni 16 ya kila mwaka ikiwa ni kumbukizi ya watoto waliouwawa mjini Soweto nchini Afrika ya kusini mwaka 1976.