Buha FM Radio

Kasulu yanufaika na ruzuku ya majiko banifu

17/03/2026, 18:45

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaack Mwakisu wakati akikata utepe kuashiria uzinduzi wa majiko banifu ya ruzuku katika Kata ya Rusesa wilayani humo. Picha na Mwandishi wetu.

“Majiko haya mkayatumie vizuri na serikali imetoa kwa gharama kidogo isiwe sababu ya kuyapeleka kwingine watu hao nikiwabaini nitawashughulikia” Amesema Mwakisu.

Na; Mwandishi wetu

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaack Mwakisu, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametekeleza ahadi ya kuhakikisha wananchi wanafurahia na kutumia nishati safi ndani ya siku 100 za uongozi wake.

Kanali Mwakisu amebainisha hayo Machi 16, 2026, wakati wa uzinduzi wa majiko banifu ya ruzuku katika Kata ya Rusesa, Wilaya ya Kasulu, ambapo amesema bei ya jiko dukani ni Sh 58,650, lakini Serikali imelipia Sh 51,000, hivyo wananchi watapata jiko hilo kwa Sh 7,650 pekee kupitia mpango wa ruzuku ya Serikali nchini hapa.

Sauti ya Mwakisu.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaack Mwakisu akikabidhi Jiko kwa mwananchi wa Rusesa wilayani Kasulu. Picha na Mwandishi wetu.

Aidha kwa upande wake Florence Masunga ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Wanawake Wajasiriamali Tanzania (TAWEN), amesema serikali imedhamiria kuondoa matumizi ya kuni kupikia kampeni hiyo iliyoanza mwaka 2024 hadi 2036 iwe imehakikisha kila Mtanzania anapata nishati safi ya kupikia.

Sauti ya Masunga.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kasulu( CCM),Mbelwa Chidebwe amesema uwepo wao ni kuendelea kufuatilia utekelezaji wa ahadi za chama zilizotolewa katika uchaguzi uliopita, hususani kuhakikisha wakinamama wanapunguza matumizi ya kuni na kuhama katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Sauti ya Mbelwa.

Nao baadhi ya wananchi Wilyani Kasulu akiwemo Husna Kaguruki na Gumbo Kihando wameridhishwa na mpango huo ambapo wamesema majiko hayo yatawapunguzia gharama za maisha, huku wakiishukuru serikali kwa kuchangia utunzaji wa mazingira kwa kutumia kuni na mkaa kidogo.

Sauti za Wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaack Mwakisu akikabidhi Jiko kwa mwananchi wa Rusesa wilayani Kasulu. Picha na Mwandishi wetu.