Buha FM Radio

Kasulu Mji yazidi kukumbwa na kipindupindu

September 10, 2025, 7:29 am

Mratibu wa elimu ya afya kwa umma Halmashauri ya Mji Kasulu ndg. Mwita Range akiwa katika ofisi za Buha Fm kutoa elimu ya Kipindupindu kwa wananchi. Picha na Paulina Majaliwa.

“Elimu ya Kipindupindu tunaendelea kuitoa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari kutokana na ongezeko la maambukizi ya ugonjwa huu ambapo mwezi Augost kulikuwa na visa vitatu hadi leo Septemba 08 mwaka huu vimefikia visa 37 vya maambukizi ya ugonjwa huu hivyo wananchi wachukuwe tahadhari kubwa” Amesema Mwita.

Na; Paulina Majaliwa

Kutokana na kuenea kwa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindipindu kwa baadhi ya maeneo Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma wakulima wameshauriwa kuchukua tahadhari  juu ya ugonjwa huo  kwani eneo lenye uwezekano mkubwa  wa kupata ugonjwa huo.

Hayo yamebainishwa na mratibu wa elimu ya afya kwa umma Halmashauri ya Mji Kasulu ndg. Mwita Range wakati akizungumza na Buha FM kupitia kipindi cha darasa nje ya shule ambapo amesema  wakulima wengi wanatumia vyakula vya baridi pamoja na maji yasiyosafi na salama kutoka kwenye visima au madimbwi na pia kujisaidia vichakani.

Sauti ya mratibu wa elimu ya afya kwa umma Mwita Range akizungumzia Kipindupindu.

Aidha Mwita amesema kundi kubwa linaloshambuliwa na kipindupindu ni wakulima hii ni kutokana na hali ya mazingira wanayofanya kazi zao kuwa si rafiki kwa afya zao.

Mratibu wa elimu ya afya kwa umma akiratibu takwimu za kipindupindu katika katika Wilaya ya Kasulu. Picha na Paulina Majaliwa.

Pia amewataka wakulima hao kuwahi katika kituo cha afya pale mtu anapopatwa na dalili za kipindupindu kama kutapika na kuharisha kusiko kawaida ili kuokoa maisha yao na kuepusha kusambaa kwa ugonjwa.

“Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakipatwa na dalili za ugonjwa huu wanachukulia jambo la kawaida jambo linapelekea mtu kupatwa na umauti kutokana na kuchelewa kupata huduma hivyo niwaombe wananchi wachukue tahadhari mapema’’amesema Mwita.

Mtaalamu ameelekeza kuwa katika Halmashauri ya Mjii Kasulu kituo cha afya kinachotumika kutibu wagonjwa wa kipindupndi ni kituo cha afya Nyasha hii ni kutokana na kituo hicho kimewekwa maalum kwa kutibu wagonjwa wanaopatikana na ugonjwa huo.

Sauti ya Mwita akielekeza kituo kinachotumika kutibu wagonjwa wa Kipindupindu.

Amehitimisha kwa kuwataka wananchi kujiepusha na kukimbilia tiba za asili  kwani hii imekuwa ni sababu ya watu wengi kupoteza maisha yao kutokana na kuanzia kwa waganga wa kienyeji bila kufuata taratibu za kitaalamu.

Sauti ya Mwita akielekeza kutotumia tiba Asili kutibu ugonjwa wa Kipindupindu.

Kwa mujibu wa mratibu wa elimu ya afya kwa umma halmashauri ya mji kasulu Ndg. Mwita Range  amesema mpaka kufikia Septemba 08,mwaka huu takwimu zinaonyesha kuwa takribani visa 37  vya ugonjwa wa kipindupindu vimepatikana vifo 05 na waliotibiwa na kuruhusiwa ni watu 29 kutoka maeneo mbalimbali ya kata za Halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani Kigoma.