Savvy FM

Maandalizi ya uchaguzi Wilaya ya Arusha yamekamilika – DC Mkude atoa tamko

October 27, 2025, 12:15 pm

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Joseph Mkude akiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari.Picha na Jenipha Lazaro

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mheshimiwa Joseph Modest Mkude, amesema maandalizi ya uchaguzi yamekamilika katika maeneo matatu ya kampeni ambayo yanaelekea ukingoni. Aidha, ametangaza kuwa siku ya Jumatano itakuwa mapumziko kwa idara zote ili wananchi waweze kushiriki kikamilifu katika zoezi la upigaji kura.

Na Jenipha Lazaro

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Mheshimiwa Mkude amesema vyama vyote vya siasa vimepata nafasi ya kufanya kampeni kwa amani na utulivu, na kuongeza kuwa kampeni zimeendelea vizuri huku baadhi ya vyama vikitarajia kufunga kampeni zao leo na kesho. Amesisitiza pia kuwa vifaa vyote vya uchaguzi vimekwisha wasili katika maeneo husika na wako tayari kwa matumizi siku ya uchaguzi.

Sauti ya Joseph Mkude,Mkuu wa Wilaya ya Arusha

Kwa upande mwingine, DC Mkude amesema kuwa usalama umeimarishwa ipasavyo katika mkoa wa Arusha, na kufafanua kuwa hakutakuwa na maandamano kama baadhi ya taarifa mitandaoni zinavyodai. Ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesisitiza kuwa maandamano yatakayoruhusiwa ni ya kuelekea kupiga kura pekee, si vinginevyo.

Sauti ya Joseph Mkude,Mkuu wa Wilaya ya Arusha