Savvy FM
Savvy FM
October 14, 2025, 2:54 pm

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Amos Makalla, amewataka vijana nchini kuendelea kudumisha amani na utulivu kabla na baada ya uchaguzi, na kuacha kuendeshwa na mihemko ya mitandao ya kijamii inayohamasisha maandamano.
Na Jenipha Lazaro
Akizungumza na wazee wa Mkoa wa Arusha katika mkutano ulioandaliwa na Jumuiya ya Wazee na kuambatana na matembezi ya amani kwa lengo la kumuenzi Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Makalla amesema ni wajibu wa kila Mtanzania kuilinda amani iliyojengwa kwa gharama kubwa.
Katika tukio hilo, Sabas Robert kutoka Chama cha Wazee Tanzania na ambaye pia ni Msemaji wa Taifa wa chama hicho, alisoma risala mbele ya mgeni rasmi, akieleza kuwa lengo la matembezi hayo ni kuimarisha afya za wazee, kutoa elimu juu ya umuhimu wa amani na mshikamano, na kuwasihi viongozi wa dini na mila kuendelea kuhubiri amani.
Nao vijana kupitia kwa Selemani Hamis, aliyewakilisha kundi hilo, wamesema wako tayari kuhakikisha taifa linaendelea kubaki kuwa na amani, na hawako tayari kutumiwa ovyo kwa maslahi binafsi ya watu wachache.
Tukio hilo limehitimishwa kwa wito wa mshikamano wa kitaifa, huku wazee na vijana wakisisitiza umuhimu wa kushirikiana katika kuilinda amani ya nchi, hasa katika kipindi nyeti cha uchaguzi.