Mtegani FM
Mtegani FM
11 September 2025, 2:00 pm

Zanzibar. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametangaza kuwa Serikali inajiandaa kuanzisha huduma ya treni za kisasa zinazotumia njia za magari, hatua itakayokuwa ya kihistoria katika kuboresha mfumo wa usafiri wa ndani ya mji.
Na Miraji Manzi Kae
Akizungumza jana Ikulu Zanzibar katika kikao na jopo la wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini, Dkt. Mwinyi alisema kuwa treni hizo za awali zitaanzia Bandari ya Zanzibar na kufika Mchuuni, eneo linaloendelea kujengwa soko jipya la kisasa.Kwa mujibu wa Rais, utekelezaji wa mradi huo utaleta mageuzi makubwa katika sekta ya usafiri kwa kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo, sambamba na kuimarisha miundombinu ya kiuchumi na kijamii ndani ya Jiji la Zanzibar.
Dkt. Mwinyi alikumbusha historia ya usafiri wa reli visiwani humo, akieleza kuwa Zanzibar ilikuwa miongoni mwa maeneo ya mwanzo Afrika Mashariki kuanzisha huduma ya treni. Mwaka 1905, chini ya utawala wa Kisultani, ilijengwa Bububu Railway, reli ya mvuke iliyokuwa ikisafirisha abiria na bidhaa kati ya Forodhani (mjinikati) na Bububu.Hata hivyo, huduma hiyo ilisimamishwa mwanzoni mwa miaka ya 1930 kutokana na gharama kubwa za uendeshaji na kupanuka kwa matumizi ya magari.
“Baada ya zaidi ya karne moja, Zanzibar sasa inarejea tena katika historia ya usafiri wa reli, safari hii kupitia teknolojia ya kisasa na njia mpya za usafiri. Huu ni mwanzo wa safari ya kujenga Zanzibar yenye miundombinu imara na ya kisasa,” alisema Rais Mwinyi.Mradi huu ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya Awamu ya Nane katika kujenga uchumi wa kisasa, kupunguza msongamano wa magari mijini, na kuongeza ufanisi wa huduma za usafiri wa umma.