Kagera Community Radio
Kagera Community Radio
August 31, 2025, 4:26 pm

Wazawa wa wilaya ya Muleba mkoani Kagera ambao hawaishi wilayani humo lakini wana uwezo kiuchumi wameaswa kukumbuka kwao kwa kujitolea kuchangia miradi ya maendeleo ili kukuza ustawi wa jamii ya Muleba.
Na Anold Deogratias
Mkuu wa Wilaya ya Muleba mkoani Kagera Dkt. Abel Nyamhanga amewataka wananchi wilayani humo kuwalea na kuwajenga Watoto wao kuwa na tabia ya kukumbuka nyumbani kwa kuwekeza na kuweka miradi mbalimbali ya maendeleo.
DC,Nyamahanga ametoa wito huo wakati wa kupokea miundombinu ya vyumba vya madarasa, madawati na visima vya maji vilivyowezeshwa na mdau wa maendeleo ambaye ni mzaliwa wa wilaya hiyo ajulikanaye kwa jina la Mosess Kiduduye.
Amesema kuwa Muleba itajengwa na wanamuleba wenyewe hivyo utamaduni huo wa kukumbuka nyumbani ni kuunga juhudi za kampeini ya mkuu wa mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwassa ya IJUKA OMUKA ambayo inawakumbusha wanakagera kukumbuka nyumbani kwa kuwekeza Kagera.
Sauti ya mkuu wa wilaya ya Muleba Abel Nyamahanga.
Akiongea na vyombo vya habari Bw. Mosess Kiduduye amesema kuwa ameamua kukarabati vyumba vya madarasa na kuchimba visima vya maji baada ya kuona mahitaji kuwa makubwa kwenye maeneo mbalimbali.
Sauti ya mfadhili Bw. Mosess Kiduduye

Naye mratibu wa miradi hiyo Bw. Sulleiman Adam Zuku ameeleza kuwa miradi hiyo ni ukarabati wa vyumba vya madarasa katika shule tano za kata ya Muleba mjini pamoja na uchimbaji wa visima viwili vya maji kwenye vijiji viwili ambayo inathamani ya zaidi ya shilingi milioni 270 na kuwataka wananchi na wanufaika wa miradi hiyo kuitunza kwa wivu mkubwa.
Sauti ya Bw. Sulleiman Zuku mratibu wa miradi

Nao baadhi ya wanufaika wa miradi hiyo wamemshukuru mdau huyo kwa moyo wa kujitolea na kuziona shida za watu hivyo itatatua adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya maji.
Sauti ya wananchi na wanufaika wa miradi hiyo

