Kagera Community Radio
Kagera Community Radio
August 26, 2025, 6:27 pm

Wiazara ya Nishati imesaini mikataba miwili ya mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kwa msongo wa kilovoti 220 kutoka Benako wilayani Ngara hadi Kyaka wilayani Missenyi utakaowezesha mkoa wa Kagera kuungwa katika gridi ya taifa ya umeme.
Na Anold Deogratias
Mkoa wa Kagera unatarajiwa kuungwa katika gridi ya taifa ya umeme kufuatia utiaji saini wa mikataba miwili ya mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kwa msongo wa kilovoti 220 kutoka Benako wilayani Ngara hadi Kyaka wilayani Missenyi na ujenzi wa kituo cha kupooza umeme cha Benako chenye msongo wa kilovoti 220/33.
Akizungumza wakati wa utiaji saini mikataba hiyo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko ameushukuru uongozi wa shirika la umeme nchini (TANESCO) kwa kukamilisha taratibu za mikataba hiyo na kusainiwa na wakandarasi.

Aidha Dkt.Biteko ameuagiza uongozi wa TANESCO kuhakikisha unawalipa fidia kiasi cha shilingi bilioni 2.6 wananchi wote wanaotakiwa kupisha mradi ifikapo Septemba 2025.
Sauti ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nshati Dkt.Doto Biteko
Naye mkuu wa mkoa Fatma Mwassa ameishukuru Serikali kwa hatua za kutekeleza miradi hiyo na kueeleza kuwa kwa sasa mkoa wa Kagera unatumia umeme megawati 46. Megawati 31 kutoka Masaka Uganda, megawati 9 kutoka Kakagati Murongo na megawati 6 kutoka Nyakanazi Biharamulo.

Pia mkuu huyo wa mkoa ameongeza kuwa miradi hiyo itaufaisha mkoa wa Kagera kwa kuziunga Wilaya zote saba katika gridi ya taifa na umeme utakuwa wa uhakika, hivyo kuwanufaisha wazalishaji wakubwa kama kiwanda cha sukari Kagera na viwanda vingine vya kusindika zao la kahawa.
Miradi iliyosainiwa mikataba itagharimu kiasi cha shilingi bilioni 262.5 ikikamilika.