Kagera Community Radio

Mwalimu atuhumiwa kumbebesha mimba mwanafunzi

July 28, 2025, 11:36 pm

Picha ya mfano wa mwanafunzi mwenye ujauzito

Mwalimu wa shule ya sekondari ya Tunamkumbuka iliyopo kata ya Butelankuzi Halmashauri ya Bukoba, anatafutwa na jeshi la polisi baada ya kumbebesha mimba mwanafunzi wa shule hiyo aliyekuwa anasoma kidato cha nne.

Na Anold Deogratias

Mkuu wa Wilaya ya  Bukoba Erasto Yohana Siima amelitaka jeshi la polisi kumtafuta na kumkamata mwalimu wa shule ya sekondari ya Tunamkumbuka iliyopo kata ya Butelankuzi halmashauri ya Bukoba mkoani Kagera kwa tuhuma za kumpa ujauzito mwanafunzi wa shule hiyo.

Akizungumza mara baada ya kufika katika shule hiyo DC Siima amaesema kuwa mwalimu huyo alitajwa na binti huyo kuwa ndiye aliyempa ujauzito na kwamba baada ya kupata taarifa hiyo mwalimu huyo amekimbilia kusikojulikana.

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Erasto Siima

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya amewasihi wazazi na walezi kufuatilia mienendo ya watoto wao ili kuwaepusha na mimba za utotoni lakini pia amezitaka shule zote wailayani humo kufanya ufuatiliaji wa wanafunzi wa kike wawapo shuleni kwa kuwapima kila mara.

Sauti ya DC wa Bukoba Erasto Siima

Kwa upande wake mkuu wa shule hiyo Mwl, Koroso Mwita amesema kuwa Julai 21 mwaka huu walimbaini mwanafunzi huyo aliyekuwa anasoma kidato cha nne kuwa ana ujauzito wa miezi 9, lakini awali alikuwa akidai kuwa ana matatizo ya kiafya hivyo kushindwa kuhudhuria masomo.

Sauti ya mkuu wa shule Koroso Mwita

Mwananfunzi huyo amepelekwa katika kituo cha afya cha Rubale kwa ajili ya uangalizi maalum.