Kagera Community Radio
Kagera Community Radio
July 24, 2025, 11:46 pm

Kijiji cha Igurwa kilichopo kata ya Igurwa wilayani Karagwe mkoani Kagera kimerejeshewa hekari 289 zilizokuwa limechukuliwa na mwananchi mmoja kwa njia isiyo halali.
Na Anold Deogratias
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera Julius Laizer ametatua mgogoro wa ardhi baina ya kijiji cha Igurwa kata ya Igurwa na mwananchi mmoja uliodumu kwa miaka 9 na kurudisha hekari 289 za kijiji hicho.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara kijijini hapo, DC Laizer amewataka viongozi pamoja na wananchi kufuata taratibu za uuzaji na utoaji wa ardhi, ikiwemo kuwa na hatimiliki ya ardhi husika pamoja na kuidhinishwa na mkutano wa kijiji kwa ardhi ya kijiji.
Aidha mkuu huyo wa wilaya amewataka viongozi wilayani humo kutotumia madaraka yao kuwanyanyasa wananchi na kuanzisha migogoro.
Awali akitoa ufafanuzi juu ya mgogoro huo, Afisa Ardhi Wilaya ya Karagwe Bw. Alex Japhet Mpunji amesema mwananchi huyo Salvator Karabamu aliuziwa hekari 351 mali ya kijiji na wananchi 9 kinyume cha sheria, hivyo baada ya maridhiano mwananchi huyo amebakiziwa hekari 59 na hekari 289.98 zimerudi kwenye kijiji.
Nao baadhi ya wananchi wa kijiji cha Igurwa Elizabeth Damiani, Livnus Method na Telesphor Maganga wameshukuru Mkuu wa Wilaya kwa namna alivyoutatua mgogoro huo kwa njia ya maridhiano na kuomba kuendelea kutumia njia hiyo ili kupunguza kesi mahakamani na kutotumia muda mrefu.
Mgogoro baina ya uongozi wa kijiji cha Igurwa na mwananchi huyo ulianza mwaka 2016, baada ya uongozi huo kudai ardhi hiyo aliyouziwa kinyume cha sheria.
