Kagera Community Radio
Kagera Community Radio
July 2, 2025, 2:13 am

Halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoani Kagera imezindua zoezi la chanjo ya kuku, huku wataalam wa mifugo ngazi ya kata wakitakiwa kufanya kazi kwa uweledi na kwa muda uliopangwa.
Na Anold Deogratias
Wataalamu wa mifugo ngazi ya kata wataohusika katika utoaji wa chanjo ya kuku katika halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoani Kagera wametakiwa kufanya kazi hiyo kwa uweledi na kwa muda uliopangwa ili kuhakikisha lengo la serikali la uchanjaji wa mifugo linatimia.
Wito huo umetolewa na kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Bukoba, Ndugu Julius Shulla, wakati wa uzinduzi wa zoezi la ugawaji wa chanjo ya kuku kwa wataalamu wa mifugo ngazi ya kata, katika hafla iliyofanyika tarehe 1 Julai 2025, katika makao makuu ya halmashauri hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ndugu Shulla alieleza kuwa chanjo hiyo imetolewa bure na Serikali kupitia wizara ya mifugo na uvuvi, kwa lengo la kuwalinda wafugaji dhidi ya hasara zinazotokana na magonjwa ya kuku, huku akisisitiza kuwa zoezi la chanjo litafanyika kuanzia Julai 1 hadi Julai 15, 2025, na kila afisa mifugo anatakiwa kutekeleza jukumu hilo kwa uaminifu na weledi mkubwa.
Sauti ya Julius Shulla kaimu mkurugenzi halmashauri ya wilaya ya Bukoba
Chanjo hiyo aina ya tatu moja imelenga kuwakinga kuku na bata dhidi ya magonjwa hatari ikiwemo mdondo (Newcastle disease), Ndui (Fowl Pox), na Mafua ya kuku (Infectious Coryza), ambayo yamekuwa yakisababisha vifo vya ndege na hasara kwa wafugaji nchini.

Katika hatua nyingine wananchi na wafugaji halmashauri ya Bukoba wametakiwa kutoa ushrikiano kwa wataalam hao ili kufanikisha zoezi hilo.
Zoezi hili ni sehemu ya kampeni ya kitaifa inayotekelezwa katika halmashauri zote nchini, na linatarajiwa kuleta matokeo chanya katika kuinua afya ya mifugo na kipato cha wafugaji.
