Butiama FM Radio

Wajasiriamali Butiama walia na bei ya mafuta

13 April 2026, 2:51 pm

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wilaya ya Butiama Samweli Burito Wambura akidhibitisha kuwa athari za kupanda kwa bei ya mafuta kumewaathiri wajasiriamali katika wilaya hiyo. Picha na Oscar Mwakipesile

Gunia moja la maembe tulikuwa tunasafirisha kwa shilingi elfu kumi sasa hivi tunasafirisha kwa shilingi elfu thelathini ukifikisha sokoni ukapandisha bei mteja anakataa anataka kununua bei aliyozoea hivyo tunajikuta mzigo unaoza kwa sababu ya kupanda kwa bei ya mafuta’Mariam Enosi Mfanya biashara wa matunda wilaya ya Butiama

Na Amos Marwa

Wajasiriamali wa wilaya ya Butiama mkoani Mara wamelalamikia kupanda kwa bei ya mafuta wakisema kumeathiri kwa kiasi kikubwa shughuli zao za biashara, hususan katika sekta ya usafirishaji wa bidhaa, Wakizungumza na Butiama fm, baadhi yao wamesema gharama za kusafirisha mizigo zimeongezeka maradufu hali inayopunguza faida na kuwalazimu kuongeza bei kwa wateja.

Wajasiriamali hao wameiomba serikali kuingilia kati na kutafuta suluhisho la kudhibiti bei ya mafuta ili kupunguza mzigo unaowakabili, Wamesema endapo hali hiyo itaendelea, biashara nyingi ndogondogo zipo hatarini kufungwa kutokana na kushindwa kumudu gharama za uendeshaji.

Sauti za wajasiliamali wilaya ya butiama wakielezea athari za kupanda kwa bei ya mafuta ulivyo athiri kazi zao.
Mariam Enos mfanyabiashara wa matunda akielezea athari za kupanda kwa bei ya mafuta zilivyo athiri biashara yake. Picha na Oscar mwakipesile

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wilaya ya Butiama Samweli Burito Wambura amethibitisha kuwepo kwa changamoto hiyo na kusema ongezeko la bei ya mafuta limekuwa kikwazo kikubwa kwa ukuaji wa sekta ya biashara. Ameongeza kuwa juhudi za haraka zinahitajika kutoka serikalini ili kuwawezesha wajasiriamali kuendelea na shughuli zao bila hasara kubwa.

Sauti ya mwenyekiti wa wafanya biashara wilaya ya Butiama Samweli Burito Wambura akielezea namna bei ya mafuta imeathiri wafanyabiashara
Adventina Justine mfanyabiashara wa vifaa vya shule na ofisini (Stationary) akielezea jinsi kupanda kwa bei ya mafuta kumeathiri biashara yake kwa kupanda kwa bei ya usafirishaji wa bidhaa zake kutoka mwanza na Musoma. picha na Oscar Mwakipesile

Aidha, sababu za kupanda kwa bei ya mafuta zinatajwa kuhusishwa na hali ya sintofahamu ya kisiasa na kiusalama duniani, ikiwemo mvutano unaoendelea kati ya Iran, Israel na Marekani. Migogoro hiyo imeathiri upatikanaji na usambazaji wa mafuta katika soko la dunia, hali inayochangia kupanda kwa bei katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.

Ester Wasanda mfanyabiashara wa mbogomboga akielezea athari za kuongezeka kwa bei ya mafuta kulivyo athiri usafirishaji wa mbogamboga kutoka mashambani kuleta sokoni kwa ajili ya walaji. picha na Oscar Mwakipesile