Bunda FM Radio
Bunda FM Radio
June 7, 2025, 10:32 am

“Mkacheze kufa ama kupona ili muweze kufuzu kwenda ligi kuu ya wanawake kwasababu mnawakilisha wilaya ya Bunda na Mkoa wa mara kwaujumla” Mkuu wa Wilaya ya Bunda Aswege Enock Kaminyoge
Na Amos Marwa
Mkuu wa wilaya ya Bunda Aswege Enock Kaminyoge amewataka wanamichezo kuongeza jitihada katika mazoezi na michezo kwa ujumla kwa kuwa michezo inaimarisha Afya na ni ajira kwa vijana.
Amesema hayo wakati akiwaaga wachezaji na viongozi wa timu ya Bunda Girls inayoelekea jijini Mwanza kushiriki mashindano ya ligi daraja la kwanza yatakayo wawezesha kufuzu katika hatua ya ligi kuu ya wanawake msimu ujao na kuwaomba waongeze jitihada ili waweze kufuzu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa timu hiyo Khalid Shani amesema wamepata muda mrefu wa kuandaa wachezaji na kuahidi mashabiki na wapenzi wa soka mkoa wa Mara kuwa watafuzu katika mashindano hayo.

Kocha wa timu hiyo Emmanuel Simion amesema timu imejiandaa vizuri kiufundi na amefuatilia wapinzani wao kwa ajili ya kukabiliana nao huku akiomba mashabiki na wadau wa soka kwendelea kuwaunga mkono.

Nae, Nahodha wa timu hiyo Angel bahati amesema kwa niamba ya wachezaji wenzake wamejiandaa vizuri na kuwatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kuwa watafanya vizuri.
Mashindano hayo yanatarajia kuanza juni 8 , 2025 jijini Mwanza na timu nne kupanda kutoka ligi daraja la kwanza na kuingia ligi kuu ya wanawake kwa msimu wa mwaka 2025/2026