Buha FM Radio
Buha FM Radio
13 April 2026, 9:35 pm

Wananchi mkoani Kigoma wafurahia huduma za madaktari bingwa katika Hospitali ya Rufaa Kabanga.
Na Sharifat Shinji
Wananchi wa Wilaya ya Kasulu na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla wamejitokeza kwa wingi katika hospitali ya rufaa Kabanga kwa ajili ya kupata huduma za kibingwa ambazo zinaendeshwa hospitalini hapo kwa wiki nzima.
Baadhi ya wananchi akiwemo Lameck Nzabuka na Gladys Emmanuel wameeleza furaha yao ya kufika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kupata huduma za kibingwa huku wakipongeza zoezi zima la utoaji huduma kwa wagonjwa wanaofika kupata matibu hospitalini hapo.

Aidha kwa upande wake Kilian Wiliam amemepongeza jitihada za hospitali hiyo kuleta kambi ya madaktari bingwa wa kada mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wenye changamoto za kiafya huku akiomba hospitali kutoa kipaumbele kwa wagonjwa wanaotoka nje ya Wilaya ya Kasulu na mkoa wa Kigoma ili wapate huduma hizo mapema.
“Kwanza tuipongeze hospitali kwa kuleta madaktari bingwa ambao watasaidia wananchi kuwatibu magonjwa mbalimbali kama tulivyosikia kwenye tangazo bila shaka tutapata huduma nzuri na kama tunavyoona watu wamekuja kwa wingi kupata huduma hii iliyotangazwa na hospitali.” Amesema Wiliamu.
Hospitali ya rufaa Kabanga imeanza kambi ya madaktari bingwa leo April 13 ambapo inatarajiwa kutamatika April 17, 2026 lengo likiwa ni kutoa huduma kwa wananchi wote wa mkoa wa Kigoma na maeneo jirani wenye changamoto mbalimbali za magonjwa yanayohitaji usaidizi wa madaktari bingwa wa kada mbalimbali.
