Buha FM Radio
Buha FM Radio
06/03/2026, 11:12

“Ili kuepuka vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa amani ni lazima familia zitekeleze malezi bora kwa watoto wao” Amesema Insp. Lupa.
Na; Irene Cherles
Mkaguzi msaidizi wa jeshi la polisi ambaye ni mratibu polisi jamii Wilaya ya Kasulu Insp. Willy Lupa amesema jukumu la ulinzi na usalama katikamaeneo ya makazi ya jamii ni lakila mtu ili kuondokana na vitendo vya uvunjifu wa amani katika familia na jamii kwa ujumla.
Amesema hayo wakati akizungumza na Buha FM Radio na kusema ili kuondokana na vitendo hivyo jamii inapaswa kuwa na malezi bora hususani katika kujenga maadili mema kwa kila wanafamilia.
Aidha mratibu huyo amewataka wananchi kujiandikisha katika daftari la mkaazi na kutoa taarifa za wageni ambao wanafika katika kaya zao ili kusaidia kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza hasa vitendo vya kihalifu.
Katika hatua nyingine Lupa amesema wanaendelea kufanya vikao na wananchi mbalimbali kutoka kata za Kagerankanda, Lungwempya na kata ya Shunguliba lengo ikiwa ni kutoa elimu ya usalama katika jamii.
Sanjali na hayo Insp. Lupa amewaasa vijana kuacha tabia za kukaa vijiweni na kubweteka bali watumie muda huo kutafuta kazi za kufanya na si kujihusisha na vitendo vya kihalifu.

Hata hivyo Insp. Lupa amewashauri wananchi kuendela kutii, kufuta na kuheshimu sheria, taratibu na kanuni ili kuepuka kuingia katika makosa mbalimbali ambayo yanaweza kuepukika na kuisisitiza jamii kushirikiana pamoja na jeshi la polisi katika utoaji wa taarifa.