Buha FM Radio
Buha FM Radio
January 28, 2026, 7:43 pm

Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma imekabidhiwa magari yaliyotolewa na Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji (IRC) ambapo yameelekezwa kusaidia Idara ya Elimu ya Awali na Msingi pamoja na Ofisi ya Mthibiti Ubora wa Shule.
Na; Sharifat Shinji
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isaack Mwakisu, amekabidhi rasmi magari mawili aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop yenye thamani ya shilingi milioni 153, yaliyotolewa na Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji (IRC) katika kambi ya wakimbizi Nyarugusu baada ya kumaliza muda wake.
Makabidhiano hayo yamefanyika Makao Makuu ya Halmashauri ya wilaya hiyo, ambapo Kanali Mwakisu amesisitiza utunzaji wa magari hayo ili yatimize malengo yaliyokusudiwa, huku akihimiza yashirikishwe idara na taasisi nyingine pale inapohitajika.

Aidha Kanali Mwakisu ameelekeza magari hayo kutumika katika Idara ya Elimu ya Awali na Msingi pamoja na Ofisi ya Mthibiti Ubora wa Shule, hatua itakayorahisisha usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za elimu wilayani humo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halamashauri hiyo CPA Francis Kafuku, ameishukuru IRC kwa msaada huo, akieleza kuwa utapunguza changamoto za usafiri na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika sekta ya elimu.

Katika hatua nyingine mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Mhe. Charles Kadogo, amesema magari hayo yataongeza tija katika usimaizi na kuboresha sekta ya elimu na kuahidi kuyatumia kwa maelekezo yaliyotolewa ili yaweze kutumika kwa muda mrefu.
