Buha FM Radio
Buha FM Radio
December 20, 2025, 4:26 pm

Hospitali ya rufaa Kabanga imehitimisha wiki ya afya katika viwanja vya kiganamo katika Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma kikiwa ni kampeni ya kurudisha kwa jamii na kuwagusa zaidi ya wananchi 700 kwa kutoa huduma bure.
Na; Sharifat Shinji
Mganga Mfawidhi wa hospitali ya rufaa Kabanga, Dkt. Bingwa wa upasuaji Ndg. Peter Kitenyi amewashukuru wananchi wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma kwa kushiriki zoezi la huduma ya vipimo bure lililokuwa linaendelea katika kiwanja cha Kiganamo Halmashauri ya Mji Kasulu.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na Buha FM Radio baada ya kutamatisha mbio za kufunga zoezi hilo la wiki ya afya Kabanga na kuwaomba wananchi kujitokeza katika hospitali ya Kabanga ili kupata huduma za kibingwa kwa magonjwa mbalimbali.
Aidha Dkt. Kitenyi amesema katika kampeni ya wiki ya afya Kabanga wamewahudumia wananchi zaidi ya 700 na wengine zaidi ya 300 kufikishwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya vipimo vikubwa vya kibingwa na kuwasisitiza watu kufanya mazoezi ili kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi wa hospitali hiyo Flora Tahondi ambaye ni katibu afya katika hospitali ya Kabanga, amesema lengo la kutoa huduma hiyo bure kwa wananchi ni kuwasaidia kuwajengea uelewa juu ya kutambua magonjwa yasiyoambukizwa huku akiwaomba kuwa na mazoea ya kufanya vipimo vya afya zao mara kwa mara.

Hospitali ya rufaa Kabanga inatoa huduma chini ya kanisa katoliki jimbo la Kigoma ambapo zoezi la kampeni ya wiki ya afya Kabanga hufanyika kila mwaka lengo likiwa ni kurudisha kwa jamii ikiwa mwaka huu limefanyika kuanzia tarehe 15 hadi 20 mwezi huu chini ya kauli mbiu isemayo “jitokeze kutokomeza magonjwa yasiyoambukizwa” ambapo zaidi ya wananchi 700 wamepata huduma katika Wilaya ya Kasulu na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla.