Buha FM Radio
Buha FM Radio
December 4, 2025, 7:30 pm

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu amewataka madiwani wenzake kutambua kuwa nafasi walizokabidhiwa ni za muda, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili waache alama chanya kwa wananchi wanaowatumikia.
Na; Emily Adam
Madiwani wateule wa Halmashauri ya wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma wamekula kiapo na kuahidi kuwatumikia wananchi wao pamoja na kusimamia na kuibua miradi mipya ya maendeleo katika maeneo ya kata zao.
Zozi la kiapo hicho limefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kagoma katika Halmashauri hiyo likienda sambamba na uchaguzi wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wialaya ya Kasulu watakaoshika nafasi hizo kwa kipindi cha miaka mitano ya utumishi wao hadi 2030.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo Katibu tawala wa Wilaya ya Kasulu Theresia Mtuwele ambapo alitaja jina la Samweli Kadogo kuwa ameshinda nafasi hiyo baada ya kupata kura 28 kati ya 29 zilizopigwa na madiwani wa Halmashauri hiyo katika kikao maalum cha uchaguzi wa viongozi huku Charles Benjameni akiwa makamu wake bada ya kushinda nafasi hiyo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu tawala mkoa wa kigoma CPSP Patrick Kigere amewapongeza madiwani hao na kuwaasa kufanya kazi zao kwa weledi na kuhakikisha wanajituma katikaukusanyaji wa mapato ya Halmashauri hiyo.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya hiyo CPA Francis Kafuku amesema vikao na maswala mengine ya eneo hilo vitakuwa vinafanyika kidigitali ambapo madiwani wote wamepatiwa vishikwambi kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo huku mafunzo ya matumizi yake yakitarajiwa kutolewa kwa wote wakiwemo madiwani wa zamani.

Halmashauri ya wilaya ya Kasulu ina jumla ya kata 21 na madiwa 28 miongoni mwao 21 ni Wanaume na 7 ni Wanawake waliowakilisha nafasi ya viti maaalumu.