Buha FM Radio
Buha FM Radio
November 30, 2025, 10:36 pm

Kituo cha kulelea watoto wenye mahitaji maalumu cha Center of Hope kimepokea misaada kutoka jumuiya ya watendaji wa serikali za mitaa (MEO`s) Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma ikiwa ni sehemu ya faraja kwa watoto hao kutokana na mahitaji waliyonayo wanapokuwa katika kituoni hicho.
Na; Paulina Majaliwa
Jumuiya ya watendaji wa serikali za mitaa (MEO`s) Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma wametoa msaada katika kituo cha Center of Hope kinacholea watoto wenye mahitaji maalumu katika Halmashauri hiyo.
Akizungumza kituoni hapo kwa niaba ya watendaji hao Afisa mtendaji ,mtaa wa Kanazi kata ya Luhita na mwenyekiti wa watendaji wa mitaa Kasulu mji Leonard Yohana amesema wadau mbalimbali wanapaswa kuwa sehemu ya faraja kwa watoto hao kutokana na mahitaji waliyonayo wanapokuwa kituoni hapo.

Aidha amewataka watendaji wa mitaa wilayani humo kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ili kujenga jamii yenye watu wanaowajibika ndani ya nchi.
“Niwaombe watendaji wa mitaa tuwe na utaratibu wa kujua mazingira ya watoto wanaotuzunguka katika mazingira yetu kwasababu sisi ndio tunaishi nao karibu hivyo tuwasaidie watoto hawa” Amesema Leonard.
Kwa upande wake mkurugenzi wa shirika la corrective calling International, meneja wa kituo cha Centre of hope na mwanasheria mkuu wa kituo hicho Rebeka Rocky amesema shirika hilo linajihusisha na uokozi,utambuzi na kusaidia watoto wenye mahitaji maalumu kwa lengo la ulinzi wa mtoto.

Katika hatua nyingine amebainisha kuwa kituo kinapokea watoto yatima na watoto wanaoishi katika mazingira magumu ambapo mpaka sasa kuna waatoto 48, baadhi yao wapo katika hatua ya awali,shule za msingi,sekondari na vyuo.
Naye kaimu mkuu wa wilaya ya kasulu Ibrahimu Mwangarume amewataka watendaji wa serikali za mitaa halmashauri ya mji kasulu kutumia mitandao ya kijamii kwa maslahi ya kujenga taifa na sio kutumia mitandao ya kijamii kuleta taharuki katika mitaa wanayoongoza.
Jumuiya ya watendaji wa serikali za mitaa Halmashauri ya mji Kasulu (MEOS) imeanzishwa mwaka 2024 ikiwa na malengo ya kuwaleta pamoja katika shughuli za kiutendaji ,kusaidiana katika shida na raha,kuwa chanzo cha ufumbuzi wa changamoto za watendaji,kupeleka mawazo,mapendekezo na changamoto katika mamlaka za juu pamoja na kuimarisha ujamaa na kusaidiana.