Buha FM Radio
Buha FM Radio
September 8, 2025, 4:12 pm

Mhe. Kanal Isack Mwakisu amewaomba wadau na wananchi kujitokeza katika mapokezi ya mbio za mwenge wa Uhuru mwaka 2025 siku ya tarehe 17 ambapo utapokelewa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu na tarehe 18 mwezi huu katika Halmashauri ya Mji Kasulu.
Na; Sharifat Shinji
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Mhe. Kanal Isack Mwakisu amewaomba wananchi wa Wilaya hiyo kujitokeza katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru unaotarajiwa kufika katika wilaya hiyo Septemba 17 mwaka huu.
Ameyasema hayo siku ya Jumamosi Septemba 6, wakati wa ufunguzi wa Bonanza lililofanyika katika uwanja wa Kiganamo katika Halmashauri ya Mji Kasulu na kusema mwenge utapitia miradi yote ya Wilaya ya Kasulu.

Aidha Mwakisu amewahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kuushangilia mwenge wa Uhuru popote utakapopita kuzindua miradi ya maendeleo katika Halmashauri zote za Wilaya ya Kasulu.
“Niwaombe sana wananchi tarehe 17 mwenge utaingia katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu utatembelea miradi yote katika Wilaya na kukesha katika viwanja vya Nyamnyusi kasha tarehe 18 tutaupokea katika Halmashauri ya Mji Kasulu hivyo tujitokeze kwa wingi kuupokea mwenge wetu wa Uhuru kisha kuushangilia popote utakapopita” Amesema Mwakisu.
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Kasulu na Mratibu wa Bonanza hilo Bi Telesia Mtewele amesema lengo la kuandaa Bonanza ni kuhamasisha wananchi kujitokeza katika mapokezi ya mbio Za Mwenge ili Wilaya iweze kufanya vizuri Kimkoa na kitaifa kwa Ujumla.

Katika hatua nyingine Mwl. Elisha ambaye ni mdau na mwandalizi wa mbio za mwenge Katika Wilaya ya Kasulu amesema mwenge wa uhuru unakuja kumulika miradi yote iliyopo katika Wilaya ya kasulu huku akiwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika mapokezi pamoja na kushiriki uchaguzi mkuu mwaka huu.

Mwenge wa Uhuru 2025 unatarajiwa kuwasili katika Wilaya ya Kasulu mnamo tarehe 17 ambapo utaanzia Halmashauri ya wilaya ya Kasulu na tarehe 18 utawasili katika Halmashauri ya Mji Kasulu na kufanya ukaguzi wa Miradi yote iliyopo katika Halmashauri ya Mji Kasulu.