Buha FM Radio

Shida ya afya Kagerankanda kubaki historia

May 24, 2025, 10:24 pm

Pichani ni baadhi ya wananchi wakiendelea na shughuli za usafishaji wa eneo la ujenzi wa kituo cha afya katika eneo la kata ya Kagerankanda katika Halmashauri ya wilaya ya Kasulu. Picha na Ajomba Lukumba.

Wakazi wa kata ya Kagerankanda katika halmashauri ya Wilaya ya Kasulu wameombwa kuendelea kushirikiana na viongozi ili kukamilisha kwa haraka zoezi la ujenzi wa kituo cha afya cha kimkakati katika eneo hilo.

Na: Sharifat Shinji

Mganga mkuu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma Dkt. Chacha Tubet amewashukuru wananchi wa Kijiji cha Kagerankanda kwa kujitolea katika zoezi la uandaji wa eneo la ujenzi wa kituo cha afya katika Kijiji hicho na kuwaomba kuendelea kujitolea na kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa.

Ameeleza hayo wakati alipotembelea katika eneo la ujenzi wa kituo cha afya katika Kijiji cha Kagerankanda na kuwaeleza wananchi wa Kijiji hicho kuwa taratibu zote zimeshafanyika za kupata pesa ili ujenzi uanze mara moja.

Sauti ya Dkt. Chacha Tubet akizungumza na wananchi waliopo katika eneo litakalojengwa kituo cha afya.

Aidha Dkt. Tubet amewaeleza wananchi namna wataalamu wa wajengo watakavyopangilia kituo kicho kikae kwa mpangilio upi huku akiwasisitiza kuendelea kushirikiana na viongozi ili kuhakikisha zoezi hilo linakamilika katika hatua za awali itakapofika June 30 mwaka huu.

Sauti ya Dkt. Chacha Tubet akiwaeleza wananchi namna wataalamu watakavyoamua kupangilia majeno ya kituo cha afya yatakavyokaa.
Wananchi wa kagerankanda wakiendelea na zoezi la kusafisha eneo la ujenzi wa kituo cha afya cha kimkakati. Picha na Ajomba Lukumba.

Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji cha Kagerankanda Ndg. Sebas Bonifas ameeleza mbele ya Mkganga mkuu wa Halmashauri ya Wilaya hiyo shughuli zilizofanywa na wananchi katika kuhakikisha eneo la kujenga kituo cha afya linakamilika Pamoja na ukusanyaji wa mawe kwa ajiri ya utekelezaji wa ujenzi huo kwa kutumia nguvu ya wananchi wa eneo hilo.

Sauti ni Mtendaji wa kijiji cha Kagerankanda akizungumza namna wananchi walivyojitolea katika zoezi la kuandaa eneo la ujenzi wa kituo cha afya.

Kata ya Kagerankanda imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya vituo vya afya Pamoja na zahanati katika maeneo hayo na kupelekea kutembea umbali mrefu kufata huduma za afya, hivyo serikali imejipanga kushirikiana na wananchi ili kuhakikisha kituo cha afya cha kimkakati kinakamilika katika eneo hilo.