Buha FM Radio
Buha FM Radio
May 12, 2025, 8:32 pm

Wananchi katika halmashauri ya Wilaya ya Kasulu wahimizwa kuendelea kushirikiana na na jeshi la polisi kuripoti matukio na vitendo vyote vya uharifu ili kuiweka jamii katika misingi ya kiusalama wa maisha na mali zao.
Na: Irene Charles
Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi na Mratibu wa Polisi Jamii Wilaya ya Kasulu Inspk. Willy Lupa amesema mtu yeyote au vikundi vya ulinzi shirikishi vikimkamata muhalifu vitanatakiwa kumpeleka kituo cha polisi na siyo kujichukulia sheria mkononi.
Amesema hayo leo wakati akifanya mahojiano na Buha FM redio katika kipindi cha “Darasa nje ya shule” na kueleza kuwa mtu akifanya kosa kila mtu ana wajibu wa kumkamata ili akapatiwe adhabu kulingana na sheria.
Aidha Insp Lupa aliongezea kwa kusema “kwa mtu ambaye anakuuliza kuwa wewe unanikamata kama nani utamjibu kwa mujibu wa sheria inayoeleza kukukamata kwa kutenda kosa la jinai mbele yangu hivyo ninawajibu wa kukukamata na kukupeleka sehemu husika”.

Wakichangia kwa njia ya simu, baadhi ya wananchi wamesema utoaji wa taarifa umekuwa mgumu kutokana na hofu ya kutoa taarifa katika jeshi la polisi kwani mtu anapotoa taarifa ya tukio wamekuwa wakishikiliwa, hivyo wameomba kupatiwa elimu juu ya mtoa taarifa kupelekwa kituo cha polisi.
Akijibia swali hilo Inspk. Willy amesema kuwa hizo ni dhana potofu taarifa zinatoka kwa wananchi hawawezi kumtumia mtoa taarifa kama mhalifu hivyo amewaomba wananchi kutoa taarifa ili kufichua maovu kwenye jamii na usalama wao utakuwa chini ya mikono ya polisi.
Kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu Inspk. Lupa amewaomba wananchi kudumisha amani na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi pale wanapoona kuna vitendo vya uvunjifu wa amani wanatakiwa kutoaa taarifa na kujiepusha kutumika katika kuleta vurugu.
Polisi jamii ni mkakati na falsafa ya kuunda sera kwa misingi ya dhana ya kushirikiana na kusaidiana na jamii ili kudhibiti uhalifu na kupunguza hofu, huku wajumbe wa jamii wakisaidia kubaini na kutambua watuhumiwa, kusimamisha ghasia na kupeleka kero za jamii katika vyombo vya dola wakiwemo polisi jamii.
