Buha FM Radio
Buha FM Radio
May 12, 2025, 7:37 pm

“Wanaume simamieni chakula katika familia ili watoto wenu wawe na afya bora kwa sababu watoto wanakua kila siku na wanahitaji kula chakula chenye virutubishi vyote ili wakue vizuri” Amesema Kimambo.
Na: Paulina Majaliwa
Wanaume katika Halmashauri ya Mji Kasulu wameshauriwa kushirikiana na wenza wao katika uandaaji wa chakula ili kuepukana na utapiamlo na magonjwa kwa watoto na familia kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Afisa Lishe wa Shirika la Kilimo na Chakula Duniani FAO Bi. Stella Kimambo katika maadhimisho ya miaka 80 ya FAO yaliyofanyika kata ya Nyasha katika halmashauri hiyo mkoani Kigoma ambapo amesema ushiriki wa wanaume katika kuandaa chakula itasaidia ulaji wa mlo kamili katika familia.
Aidha amesema kuwa ili kujenga jamii yenye afya bora wanaume pia wana wajibu wa kushiriki katika kuandaa na kupangilia ulaji wa chakula bora katika jamii ili kuimarisha afya kwa familia.
“Nawasihi wanaume simamieni chakula katika familia ili watoto wenu wawe na afya bora kwa sababu watoto wanakua kila siku na wanahitaji kula chakula chenye virutubishi vyote ili wakue vizuri” amesema Stella Kimambo.

Kwa upande wake afisa lishe katika halmashauri ya Mji Kasulu Ndg. John Sabatele amesema kuwa jamii inatakiwa kuepuka ulaji wa vyakula vyenye sukari kwa wingi na mafuta kwa wingi ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukizwa kama vile kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya mishipa.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema kuwa wataendelea kutumia elimu waliyoipata kupitia mafunzo hayo ya lishe kutoka katika shirika la FAO pia wamesema watakuwa mabalozi kwa wananchi wengine ambao hawajabahatika kupata elimu hiyo.
Chakula bora ni muhimu kwa binadamu kwani huupatia mwili nishatti,lishe na virutubishi mbalimbali ili kuuwezesha mwili kufanya kazi kwa ufanisi hivyo ni vyema kuzingatia ulaji bora wa chakula ili mwili uweze kupata mahitaji yote ya lishe.
