Buha FM Radio
Buha FM Radio
April 27, 2025, 1:34 pm

“Niwasihi mnavyofurahi kukopa fedha hizi na kurejesha iwe hivyo ili kupata nafasi ya kukopa zaidi kwa sababu kunabaadhi ya vikundi vilikopa awamu iliyopita ilishindwa kurejesha kutokana na kutokuwa na matumizi sahihi ya fedha hizo”
Na Paulina Majaliwa
Mbunge wa jimbo la Kasulu Mjini Prof. Joyce Ndalichako amewaomba wanufaka wa mikopo ya serikali ya asilimia kumi ya mapato ya ndani kutumia kwa usahihi pesa hizo ili kuweza kuendesha miradi waliyoanzisha na kurejesha mikopo kwa wakati ili kuwapa nafasi wananchi wengine kukopa fedha hizo.
Amesema hayo April 26,2025 wakati akikabidhi hundi ya mikopo hiyo na vifaa kwa vikundi mbalimbali katika viwanja vya Halmashauri Mji Kasulu na kusema kuwa baadhi ya vikundi vimekuwa vikishindwa kurejesha pesa hizo kutokana na kutoendeleza miradi waliyoanzisha wakati wa kukopa mikopo hiyo.
Aidha amesema vikundi ambavyo havijapata mkopo huo ni kwa sababu havijakidhi vigezo hivyo waendelee kuboresha taarifa zao ili wapate mikopo kwa awamu nyingine kwani mikopo hii ni ya mwendelezo pia wafikishe taarifa zao kwa mkurugenzi wa halimashauri Mji Kasulu ili taarifa zao zitambulike.
Kwa upande wao baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo wilayani Kasulu wameishukuru serikali kwa kuwapatia mikopo hiyo kwani itawasaidia katika kuendeleza miradi mbalimbali kama vile biashara,kilimo na ufugaji pamoja na kuinua uchumi wao binafsi kutokana na elimu waliyoipata na kuahidi kuwa watafanya kazi kwa bidii ili kujikwamua kiuchumi.
Mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halimashauri nchini Tanzania ni sehemu ya juhudi za serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi kwa makundi maalum ikiwa ni pamoja na wanawake,vijana na watu wenye ulemevu na fedha hizi hutolewa kwa vikundi vilivyosajiliwa ambapo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kwa awamu hii imetenga bajeti ya kiasi cha shilingi milioni 514 ambapo imetoa mikopo yenye thamani ya kiasi cha shilingi milioni 433 kwa vikundi 32 vyenye jumla ya wanufaika 230 waliokizi vigezo vya kupokea mikopo hiyo.
