Smile FM Radio

Bilioni 19 kujenga stendi mpya Manyara

July 25, 2025, 8:08 am

Picha ya mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga akiongea wakati wa kusaini mkataba wa ujenzi wa stendi ya mabasi Manyara

Ujenzi utakaogharimu shilingi za kitanzania takribani bilioni 19, utasaidia kukuza uchumi kutokana na fursa mbalimbali za kibiashara zitakazojitokeza.

Na Linda Moseka

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Cuthbert Sendiga amewaasa viongozi wa serikali ndani ya halmashauri ya mji wa Babati kuacha tabia ya kujilimbikizia vibanda vya stendi pindi ujenzi wa stendi mpya utakapokamilika, ili kutoa fursa sawa kwa wote kwani kibanda kimoja kinapaswa kumilikiwa na mtu mmoja pekee.

Sendiga ameyasema hayo leo tarehe 24 mwezi wa 07 mwaka 2025 kwenye eneo la stendi mpya iliyopo halmashauri ya mji wa Babati katika zoezi la kusaini mkataba wa ujenzi wa kisasa wa stendi hiyo kupitia mfuko wa mradi wa uboreshaji wa miundo mbinu ya miji ya Tanzania kupitia ofisi ya Raisi TAMISEMI, utakaogharimu shilingi za kitanzania takribani bilioni 19, ambapo mkuu wa mkoa amesema ujenzi huo utasaidia kukuza uchumi kutokana na fursa mbalimbali za kibiashara zitakazojitokeza.

Sauti ya mkuu wa mkoa wa manyara

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Babati Shabani Mpendu wakati akisoma taarifa ya mradi huo amesema ujenzi wa stendi ya kisasa utatekelezwa na mkandarasi kwa kipindi cha miezi 15 na tayari mkandarasi amesaini mkataba tayari kuanza ujenzi.

Aidha Mpendu ameeleza mchanganuo wa maboresho ya stendi hiyo pindi itakapokamilika kuwa vitajengwa vibanda 60 vya biashara, vibanda vya mama lishe 12, vibanda vya kukatia tikiti 16, vibanda vya walinzi 3, kibanda cha kukusanyia taka 1, ambapo vibanda hivyo vya biashara vinatarajiwa kuwanufaisha wananchi kiuchumi.

Sauti ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Babati Mjini

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Maisaka A uliopo mjini Babati Hussein Mkindi ameishukuru serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Raisi Dokta Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha hizo ndani ya mji wa Babati na kumsihi mkandarasi afanye kazi yake kwa ufasaha, itakayolingana na thamani ya fedha iliyotolewa.

Sauti ya mwenyekiti wa mtaa wa Maisaka A

Mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya miji ya Tanzania unaifanya halmsahauri ya mji wa Babati kuwa kati ya halmashauri 15 zilizofikiwa na mradi huu na licha ya stendi mpya ya mabasi lakini pia mradi utahusisha ujenzi wa barabara za lami nzito zenye urefu wa kilomita 4.7.