Kagera Community Radio

Wenyeviti wa vijiji Kyerwa waonywa uuzaji wa ardhi ya kijiji

September 27, 2025, 4:59 pm

Mkuu wa wilaya ya Kyerwa Bi.Zaituni Msofe

Wenyeviti wa vijiji wilayani Kyerwa mkoani Kagera wameonywa juu ya kujichukulia maamuzi ya kuuza ardhi ya kijiji bila kuwashiriki wananchi kupitia mikutano mikuu ya vijiji.

Na Anold Deogratias

Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera Zaituni Msofe, amewataka wenyeviti wa vitongoji na vijiji kuacha taibia ya kuuza ardhi ya kijiji bila ya mikutano ya vijiji kwani ardhi ya kijiji ni mali ya wanakijiji.

Akizungumza katika kata ya Nyaruzumbura kwenye ziara ya kusikiliza kero za wananchi Bi.Msofe amesema uuzaji wa ardhi bila ushirikishwaji wa wananchi ni kinyume na sheria lakini pia ndicho chanzo cha migogoro ya ardhi kwenye jamii.

Mkuu wa wilaya ya Kyerwa Bi.Zaitun Msofe

Aidha ameyataka mabaraza ya ardhi wilayani humo kutatua migogoro ya ardhi kwa kuweka mipaka ili kuondoa migogoro ya ardhi kwenye jamii na kwamba kujirudia kwa kesi za migogoro ya ardhi ni kutokana na kutowekwa kwa mipaka ya kudumu inayotenganisha maeneo.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Kyerwa Bi.Zaituni Msofe

Wananchi wa kata ya Nyaruzumbura wakimsikiliza mkuu wa wilaya.

Katika hatua nyingine mkuu wa Wilaya ya Kyerwa amewasisitiza wafugaji kuendelea kushiriki kikamilifu katika zoezi la utambuzi na kuchanja mifugo, zoezi ambalo linaendelea katika Kata zote ikiwa ni pamoja na kudhibiti mifugo inayozurura katika maeneo ambayo sio ya kufugia.

 Sauti ya mkuu wa wilaya ya Kyerwa Bi.Zaituni Msofe

Itakumbukwa zoezi la utambuzi wa mifugo pamoja na utoaji chanjo kwa mifugo ili kuwakinga na magonjwa mbalimbali linaendelea nchi nzima ambapo kwa ng’ombe mmoja mfugaji anachangia shilingi mia tano ikiwa fedha nyimgine imeishawekwa na serikali.

Wananchi wa kata ya Nyaruzumbura walioudhuria mkutano wa mkuu wa wilaya.