Kagera Community Radio

Wakulima wa kahawa waaswa kanuni za kilimo bora

August 7, 2025, 6:28 pm

Zao la kahawa

Wakulima wa zao la kahawa mkoa wa Kagera wametakiwa kufuata maelekezo ya wataalamu kuhusu namna kufanya kilimo bora cha kahawa ili kunufaika zaidi na zao hilo.

Na Anold Deogratias

Wakulima wa zao la kahawa mkoani Kagera wametakiwa kufuata kanuni za kilimo bora cha zao la kahawa ili kuwezesha uzalishaji wa tani 200,000 kwa mkoa wa Kagera ifikapo mwaka 2030.

Akizungumza katika maonyesho ya wakulima Nane Nane mjini Bukoba, mkurugenzi wa Taasisi taasisi ya Utafiti ya Kahawa (TACRI), kanda ya Kagera, Dk Nyabisi Ngho,ma amesema utafiti uliofanywa kwa wakulima wa zao la kahawa mwaka 2006 kupitia taasisi hiyo ulibaini kuwa kama wakulima watafuata kanuni bora za kilimo cha kahawa mche mmoja unaweza kuzalisha kahawa safi kilo 2.5 hadi 3.5.

Mkurugenzi wa (TACRI), Kagera, Dk Nyabisi Ngho,ma akitoa elimu kuhusu kilimo cha kahawa

Amezitaja kanuni hizo hizo kuwa ni pamoja kukata matawi vizuri, kudhibiti magonjwa na wadudu, kuweka mkazo kwenye lishe ya miti ya kahawa, kufanya palizi shambani, kuhakikisha wanaondoa maotea mara kwa mara, kuweka matandazo vizuri,kumwagilia maji inapowezekana kama jua ni kali sana pamoja na kupangilia kivuli kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu.

Sauti ya mkurugenzi wa (TACRI), Kagera, Dk Nyabisi Ngho,ma

Kwa upande wake mdau wa kahawa mkoa wa Kagera Bi Amina Kashoro ameiomba serikali kuendelea kugawa michezo bora ya kahawa kwa wananchi na kufanya ufuatiliaji wa miche hiyo ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanatimia.

Sauti ya mdau wa kahawa mkoa wa Kagera Bi Amina Kashoro

Naye mmoja wa wadau wa viwanda vinavyosindika zao la kahawa Domisian Mujiri, amepongeza maonyesho hayo ya kilimo kwani yanatija kwa wananchi na wadau wa viwanda kutangaza bidhaa zao na pia wanannchi kujifunza mambo mbalimbali katika maonyesho hayo.

Sauti ya mdau wa viwanda vya kahawa Domisian Mujiri

Kwa sasa inakadiriwa kuwa mkoa wa Kagera unazalisha tani elfu 60 za kahawa kwa mwaka huku ikikadiliwa kuwa mapato yanayotokana na kahawa ni shilingi bilioni 256 na lengo ni kupata mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 900 ifikapo mwaka 2030.

Shamba la kahawa