Kagera Community Radio

Wananchi Kagera washauriwa kufuga samaki kisasa

July 13, 2025, 2:40 pm

Vizimba vya kufugia samaki

Wananchi mkoani Kagera wameshauriwa kujikita katika teknolojia mpya ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba  ili kuzalisha samaki kwa wingi na kujipatia kipato.

Na Anold Deogratias

Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa amewashauri wananchi mkoani Kagera kujikita katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ili kuweza kuongeza uzalishaji wa samaki na kujipatia pato la kutosha kutokana na ufugaji huo.

Mwassa amesema hayo katika ofisi za mkuu wa mkoa manispaa ya Bukoba, wakati akizungumza na vijana zaidi 140 kutoka halmashauri zote za mkoa wa Kagera ambao waliokutanishwa mjini Bukoba kupatiwa elimu juu ya ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba.

Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa

Amesema kuwa ufugaji huo wa kisasa utawezesha uzalizaji wa samaki kwa wingi na kuongeza pato la mwananchi mmojamoja na mkoa kwa ujumla, ambapo pia amezitaka halmashauri zote mkoa wa Kagera kutenga fedha kwa ajili ya kuwakopesha wananchi wanaohitaji kuwekeza katika ufugaji huo wa kisasa.

Sauti ya Fatma Mwassa mkuu wa mkoa wa Kagera

Kwa upande wake Afisa uvuvi mkoa wa Kagera Efrazi Mkama ameeleza kuwa mradi huo unakwenda kupunguza gharama kwa wavuvi ambao awali walitakiwa kujigharamia wenyewe, na kwamba mpaka sasa mkoa wa Kagera una maeneo 12 kwa ajili ya ufugaji huo na tayari vimba 52 vimesimikwa.

Sauti ya Efrazi Mkama Afisa uvuvi mkoa wa Kagera

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo Emmanuel Shija Busanda na George Buberwa wamesema kuwa teknolojia ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ina manufaa makubwa kwa wafugaji wa samaki kwani inaongeza uzalishaji wa samaki kwa wingi.

Sauti za washiriki wa mafunzo ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba

Washiriki wa mafunzo ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba

Imeelezwa kuwa kizimba kimoja chenye ukubwa wa mita za mraba 256 kina uwezo wa kuzalisha tani 14 kwa muda wa miezi saba na tayari mikopo ya shilingi bilioni 1.5 imetolewa na Serikali kwaajili ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba na dhana bora za uvuvi mkoani Kagera.

Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa akipokea maelezo kutoka kwa wataalum juu ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba