Kagera Community Radio
Kagera Community Radio
June 14, 2025, 9:45 am

Wakazi mkoani Kagera wamesema wamekua wakiingiza kipato kinachowawezesha kujikimu kwa biashara ya wadudu aina ya senene
Na. Elisa Kapaya
Idadi kubwa ya wakazi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kagera wamekiri kupata fursa kubwa ya kipato kutokana na kufanya biashara ya wadudu aina ya senene.
Wakizungumza katika mahojiano maalum na Kcr fm wakazi hao akiwemo Mektrida Leonard wamesema katika msimu wa senene wamekua wakipata kipato kinachowawezesha kujikimu na kupata mahitaji yao pamoja na kulipa ada za watoto shuleni.
Mtaalamu wa masuala ya lishe Mery Christian amesema senene ni chanzo bora cha protini, ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa misuli, kutengeneza tishu na seli, na kuimarisha mfumo wa kinga.

Kwa upande wake katibu tawala msaidizi upande wa uchumi na uzalishaji kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa kagera bwana Isaya Tendega amesema wadudu hao wamekua na mchango mkubwa kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuongeza mzunguko wa fedha katika kipindi cha msimu wa senene.