Teknolojia ya kisasa kilimo cha umwagiliaji yawanufaisha wakulima
Na; Mindi Joseph.
Wakulima katika skimu za kilimo cha umwagiliaji wametaja kunufaika na teknolojia ya kisasa ambayo ni mbadala wa matumizi ya rasimali maji.
Baadhi ya wakulima kutoka Kiwere na Mafuruto, wamesema wamenufaika na teknolojia hiyo maarufu kwa jina la kinyonga teknolojia ambayo inasaidia kupata mazao mengi kwa kutumia maji kidogo huku wakiomba serikali kuwasaidia kuhusu pembejeo.
News Express imefanikiwa kuzungumza na Mhandisi wa Umwagiliaji Onesmo Kahogo, ambapo amesema teknolojia hii inasaidia kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya Tabianchi, kwani inamsaidia mkulima kupima kiwango cha maji anayohitaji kutumia shambani na haina madhara kwa mazao.
Mhandisi Kahogo amesema Teknolojia hii imesaidia kupungua kwa migogoro ya maji kwa wakulima na inampa mkulima nafasi ya kufanya shughuli nyingine za uzalishaji pamoja na kutumia maji yanayotosha kumwagiliwa katika eneo husika na kwa kiasi ambacho mkulima anakuwa amejipimia kulingana na mahitaji ya maji kwa wakati huo na teknolojia hiyo kutumia maji kidogo inasaidia pia matumizi madogo ya pembejeo, kutokana na kwamba hazisombwi na maji shambani.