Sokwemtu hatarini kutoweka katika Hifadhi ya Taifa Gombe
Buha FM Radio

Sokwemtu hatarini kutoweka katika Hifadhi ya Taifa Gombe

January 16, 2026, 7:04 pm

Sokwemtu akiwa katika Hifadhi ya Taifa Gombe mkoani Kigoma: Picha na Prosper Kwigize.

Shughuli za binadamu ikiwemo kilimo, uchomaji wa mkaa, ukataji miti kwa ajili ya nishati kuni pamoja na naongezeko la makazi ya watu katika maeneo ya Hifadhi ya Taifa Gombe mkoani Kigoma, zimetajwa kusababisha mabadiliko ya Tabianchi katika eneo hilo hali inayopelekea sokwe kutoweka katika maeneo hayo.

Na: Prosper Kwigize

Wakazi wa maeneo ya Hifadhi ya Taifa Gombe iliyopo katika Mkoa wa Kigoma kando ya Ziwa Tanganyika wamesema kuna hatari ya kutoweka kabisa kwa Sokwe mtu katika hifadhi hiyo kutokana na shughuli za binadamu zinazofanyika katika maeneo ya misitu ya Hifadhi hiyo.

Wameeleza hayo wakati wakizungumza na Buha Fm Radio wakati mwandishi wa masuala ya mazingira Prosper Kwigize kifanya utafiti wa kufahamu sababu zinazopelekea Sokwe mtu kupungua katika Hifadhi hiyo ambapo imeelezwa Sauti za ndege na sokwe zimekua adimu tofauti na miaka ya nyuma.

Hifadhi ya Taifa ya Gombe Stream Ni moja ya hifadhi ndogo zaidi hapa nchini Tanzania, ikiwa na eneo la takribani 52 km², lakini ni maarufu sana duniani kutokana na kuwa kituo cha utafiti wa sokwe wa asili, Hifadhi hii ilianzishwa rasmi mwaka 1968 lakini ilipata umaarufu mkubwa kutokana na kazi za mtafiti mashuhuri Dr. Jane Goodall, ambaye alianza utafiti wake wa sokwe  mwaka 1960. Utafiti wake uligundua tabia za kipekee za sokwe, kama vile matumizi ya zana na maisha yao ya kijamii, jambo lililobadilisha namna binadamu wanavyowaelewa sokwe.

Sokwemtu akiwa katika Hifadhi ya Taifa Gombe mkoani Kigoma: Picha na Prosper Kwigize.

Katika takwimu za hivi karibuni Tanzania inakadiriwa kuwa na sokwe wapatao 2500. Asilimia 75 kati yao wanaishi nje ya maeneo yaliyohifadhiwa. Hii inawaweka katika hatari kubwa ya kuendelea kupotea.Hata hivyo shirika la takwimu la Data setilaiti limeonyesha Tanzania imepoteza zaidi ya hekta milioni mbili za misitu katika miongo miwili iliyopita, sehemu kubwa ya hasara hii iko karibu na Ziwa Tanganyika na Milima ya Gombe jambo lililochangia kuendelea kupoteza mazalia na malisho ya sokwe katika Hifadhi hiyo.

Kulingana na mwanaikolojia Silla Mbise kutoka mamlaka ya hifadhi za Taifa TANAPA alisema mnamo 1980, Gombe ilikuwa na sokwe wapatao 300, na Mnamo 2023, Sokwe 90 walibakihuku leo hii wakiwa wamasalia sokwe 85 pekee katika Hifadhi hiyo.

Inatajwa kuwa Sokwe hao wamebakisha njia moja tu ya uhamiaji wao pamoja na wanyamapori wengine ambapo inatajwa, Gombe na misitu ya Burundi ndio hutumika kuhama kwa sokwe hao, licha kwa njia hiyo pia kuendelea kuhribiwa na kilimo, uchomaji wa mkaa, na makazi ya watu kama alivyoeleza wasiwasi wake kuhusu hali hiyo, Afisa wa maliasili kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Bw. Vicent Muhezi anathibitisha kuwepo kwa changamoto ya uhifadhi wa misitu.

Aidha mabadiliko ya tabianchi kama halijoto kali, mimea vamizi, na misitu iliyogawanyika  yametajwa kama kichocheo kinachoongeza hatari, ya idadi ya sokwe, kukosa majike au madume kwa ajili ya uzazi na kuongeza migogoro kati yao.

Sokwemtu akiwa katika Hifadhi ya Taifa Gombe mkoani Kigoma: Picha na Prosper Kwigize.

Ujangili pia ni tishio licha ya mamlaka ya wanyamapori kuchukua hatua mbalimbali kama alivyoeleza Alfred Msangi afisa wa wanyamapori kutoka wilaya ya Kigoma kwa kukili kuwa doria na elimu kwa umma ndiyo inayotumika kunusuru wanyamapori na makazi ya sokwe hao.

Hata hivyo, juhudi za uhifadhi zinakabiliwa na changamoto,kufuatia mabadiliko ya sera ya Rais wa Marekani Donald Trump ya kufuta ufadhili wa USAID, baadhi ya miradi ya urejeshaji nchini Tanzania imesimama bila rasilimali za kifedha za awali. Lakini bado kuna matumaini kutoka serikali ya Tanzania kupitia mamlaka za wanyapori na uhifadhi wa mazingira kuweka mipango ya upandaji miti upya ili kendelea kulinada mazingira na viumbe vinavyotegemea mazingira hayo.