Buha FM Radio
Buha FM Radio
December 24, 2025, 7:18 pm

Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani Wilaya ya Kasulu, ASP Partrick Damasi amesema wakati wa sikukuu wazazi wanapaswa kuwalinda watoto wao ili wasipate changamoto ya kupotea.
Na; Sharifat Shinji
Wananchi wilayani Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kuzingatia sheria za usalama barabarani wakati wa kufurahia sikukuu za Krismasi na mwaka Mpya ili kuepukana na ajali zinazoweza kujitokeza wakati wa sharehe hizo.
Tamko hilo limetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani Wilaya ya Kasulu, ASP Partrick Damas wakati wa mahojiano maalumu na Kituo cha Buha Fm Radio, na kuwasisitiza madereva wa vyombo vya moto kuepuka kutumia vyombo hivyo wakati wakiwa katika hali ya ulevi.
Aidha amesema siku za sikuku kitengo cha usalama barabarani kimejipanga kukabiliana na hali yoyote ya uvunjifu wa sheri za barabarani na kuahidi kuwalinda dhidi ya ajali raia watakaotoka kwenda kusherehekea hasa katika Senta zote za Wilaya ya Kasulu.
Katika hatua nyingine Damas ametoa rai kwa wazazi kuhakikisha wanawalinda watoto katika sikukuu ili kuepusha changamoto za watoto kupotea na kutoa maelekezo ya wazazi kuwaeleza watoto namna ya kujisaidia watakapopata changamoto hasa kwa kuwafuata Askali bila kuogopa.

Ripoti ya Jeshi la Polisi ya mwaka 2024 iliyowasilishwa na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia alisema kati ya Januari na Desemba mwaka 2024, nchi ilirekodi jumla ya ajali 1,735 ambapo ajali 1,198 zilisababisha vifo vya watu 1,715 na wengine 2,719 kujeruhiwa ikiwa ni asilimia 97 ya ajali hizo zilisababishwa na makosa ya kibinadamu huku sababu zinazoongoza zikiwa ni uzembe, kuendesha gari kwa uzembe na mwendo kasi ambao kwa pamoja unachangia asilimia 73.7 ya ajali zote.