Buha FM Radio
Buha FM Radio
December 13, 2025, 3:25 pm

Wakulima wilayani Buhigwe kupitia kwa mbunge wa jimbo la Buhigwe Prof. Pius Yanda wamenufaika na mafunzo ya mikopo kutoka Taasisi ya kifedha ya Bank ya CRDB kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo kupitia mikopo hiyo.
Na; Sharifat Shinji
Wakulima katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe wamehudhuria semina ya mafunzo ya kilimo iliyoandaliwa na Bank ya kibiashara CRDB kwa lengo la kujifunza maswala ya mikopo kwa ajili ya kilimo cha mazao ya chakula katika Halmashauri hiyo.
Wakizungumza na Buha FM Radio baadhi ya wakulima waliohudhulia semina hiyo wamesema elimu walioipata itaenda kuwasaidia hasa katika maswala ya mikopo na kuiomba serikali iwasaidie kukidhi vigezo vya kupata mikopo hiyo ili waweze kunufaika nayo.
Aidha kwa upande wake muwezeshaji wa mafunzo hayo Peter Christopher Meneja wa CRDB makao makuu na msimamizi wa mradi wa kilimo cha mazao lishe amesema malengo ya kuwafikia wakulima wa mazao ya chakula wa Halmashauri hiyo ni kuongeza usalama wa chakula na kuwezesha uhimilivu wa mabadiliko ya tabia ya nchi.

Muwezeshaji huyo ameongeza kwa kusema mradi huo umelenga kuwafikiwa wanufaika zaidi ya milioni 6 wa moja kwa moja na wasio wa moja kwa moja ndani ya kipindi cha miaka 20 ya utekelezaji wa mradi huo huku wakiwa wamewafikia zaidi ya wanufaika laki tano na kutoa pesa zaidi ya bilioni 100 kwa wanufaika hao.
Katika hatua nyingine Kaimu Mkurugenzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe Hamza Mnaliwa amesema ili wakulima wapige hatua katika shughuli zao za kilimo ni lazima kupata mikopo midogo midogo ili kuwasaidia kuendesha kazi zao za kilimo huku akiwataka wakulima kuzingatia uaminifu wa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Mbuhge wa Jimbo la Buhigwe na yamewaleta pamoja maafisa wa CRDB kwa ajili ya kutoa elimu ya mikopo kwa wakulima wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe, Madiwani, watendaji wa kata na maafisa ugani kutoka kata zote za Halamashauri hiyo kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa Buhigwe kupata mikopo katika shughuli za kilimo.